Mchezaji soka kutoka Rwanda Mike Tresor Ndayishimiye alitajwa kuwa mshindi wa tuzo ya Ebony Shoe, inayo watambua wachezaji bora zaidi wa kiafrika au wenye asili ya kiafrika, katika ligi ya Ubelgiji.
Ndayishimiye, anachezea klabu ya Genk na ametajwa kuwa katika fomu nzuri zaidi msimu huu akitoa usaidizi 23 wa magoli katika mechi 35, na kujifungia magoli 8 binafsi.
Alizaliwa mjini Antwerp na baba kutoka Burundi, ambaye pia alikuwa mchezaji soka maarufu na mama yake kutoka Rwanda.
Amekuwa akichezea timu ya taifa ya Ubelgiji ya U-20, japo bado anaruhusiwa kuchezea Rwanda, kwa mujibu wa mtandao wa News Times Rwanda.
Tuzo hiyo ijulikanayo kama Soulier d’Ebene, ilianzishwa 1992 na tangu hapo imetawaliwa na wachezaji kutoka Afrika magharibi.
Mara mbili tu imewahi kunyakuliwa na wachezaji wa Afrika Mashariki, 2007, ilipokwenda kwa Mohammed Chite wa Anderlecht, mwenye uraia wa Burundi na Rwanda, na 2019, ilipokwenda Tanzania kwa Mbwana Samatta, wa Genk.