Wachezaji wa Atletico Madrid / Photo: AA

Klabu ya mpira wa miguu ya Super Lig Uturuki, Besiktas itakutana na Klabu ya La Liga Hispania Athletico Madrid, katika mechi ya kirafiki mjini Istanbul kwa ajili ya kusaidia watu walioathirika katika tetemeko la ardhi mwezi wa pili mwaka huu.

"Tunakuja Istanbul. Safari ya kucheza mchezo wa hisani kwa wale walioathiriwa na matetemeko ya ardhi," Atletico Madrid walisema kupitia ukurasa wao wa Twitter.

Besiktas ilisema kwenye tovuti yake kwamba tiketi zitaanza kuuzwa Jumapili tarehe 9, huku mapato yakitengwa kusaidia ujenzi wa baadhi ya shule katika maeneo yaliokumbwa na tetemeko hilo.

Klabu ya Uhispania ya La Liga ilithibitisha kuwa mechi hiyo itafanyika katika uwanja wa Vodafone Park, Istanbul Jumatano, Aprili 12 kuanzia saa kumi na moja na nusu saa za kimataifa (17:30GMT).

Zaidi ya watu 50,000 walikufa na watu zaidi ya milioni 1.5 wameachwa bila makao kutokana na tetemeko la ardhi iliyotokea Uturuki na Syria mapema Februari. Mamilioni ya watu katika majimbo 11 waliathirika.

TRT Afrika na mashirika ya habari