Mikataba ya wanasoka inastahili kuheshimiwa - watetezi wa  wachezaji waonya vilabu vya Ligi kuu Kenya

Mikataba ya wanasoka inastahili kuheshimiwa - watetezi wa  wachezaji waonya vilabu vya Ligi kuu Kenya

Muungano wa kutetea maslahi ya wanasoka imeonya vilabu dhidi ya kuwachukulia wachezaji kama bidhaa badala ya wanadamu.
Rais wa chama cha ustawi wa wanasoka Kenya (KEFWA) James Situma​. Picha/ (KEFWA) 

Usajili wa wanasoka ukizidi kushika kasi katika ligi mbalimbali ulimwenguni, Chama cha Ustawi wa Wanasoka nchini Kenya (KEFWA) sasa kimevionya vilabu vya ligi kuu nchini humo kuheshimu mikataba na wachezaji wake.

Shirika hilo linalolinda na kukuza ustawi wa wanasoka wa kulipwa, lilionyesha wasiwasi wake kufuatia ongezeko la visa vya vilabu kuwaachilia zaidi ya wachezaji 10 kwa mpigo na kusababisha mazingira yasiyo ya haki kwa wachezaji wa soka nchini Kenya.

Vilabu hivyo sasa vimetakiwa kushughulikia ipasavyo haki na wajibu wa wachezaji waliopo kwenye timu huku wasiwasi ukiongezeka juu ya jinsi wachezaji wanavyodhulumiwa wakati wa uhamisho haswa vilabu vikijaribu kuwasajili wachezaji wapya.

KEFWA imetoa wito kwa vilabu vya kandanda kuheshimu kandarasi za wachezaji wakati wa dirisha hili la uhamisho linaloendelea na kuwaachilia wachezaji wakati tu majukumu yote ya kimkataba yametimizwa.

Kwenye taarifa kwa waandishi, Katibu Mkuu wa KEFWA Dan Makori, amesema kuwa ni lazima ustawi na maendeleo ya kazi ya wachezaji upewe kipaumbele.

Hatuwezi kuruhusu soko la uhamisho kuwa la bure kwa wote ambapo wachezaji wanachukuliwa kama bidhaa badala ya wanadamu.

Dan Makori

Muungano huo wa KEFWA, pia umewashauri wachezaji kuwa makini katika kufahamu kanuni na masharti ya mikataba wanayosaini na vilabu ili kuepukana na balaa.

"Kwa kuelewa haki na wajibu wao, wachezaji wanaweza kukabiliana vyema na changamoto na kutokuwa na uhakika ambao mara nyingi huambatana na dirisha la uhamisho. " Alisema Makori.

"Wachezaji husaini mikataba hii kwa nia njema na wanatarajia kuheshimiwa kwani makubaliano haya sio tu yanawapa wachezaji usalama wa kifedha, lakini pia hulinda haki zao." Makori aliongeza.

Uhamisho wa wachezaji wa ligi kuu ya soka nchini Kenya umekuwa na mvuto mkubwa huku vilabu vikilenga kujiimarisha kwa minajili ya kulinyakua taji hilo kutoka Gor Mahia waliotwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka msimu uliomalizika.

TRT Afrika