Lionel Messi ameihama PSG na kujiunga na Miami ya Marekani. Picha: Getty

Rais wa PSG Nasser Al Khelaifi amemjibu Lionel Messi kufuatia matamshi ya nyota huyo wa Argentina kufuatia madai yake ya 'kutoheshimiwa ipasavyo' na PSG baada ya ufanisi wake Kombe la Dunia.

Haya yanajiri baada ya kauli za Messi wakati wa mahojiano ya hivi karibuni kuwa hakuandaliwa sherehe katika uwanja wa PSG tofauti na nyota wengine wa Argentina walivyopongezwa hadharani na vilabu vyao.

Mnamo Desemba 2022, Messi aliongoza Argentina kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya fainali dhidi ya Ufaransa.

Messi aliliambia jarida la ESPN Argentina kuwa "nilikuwa mchezaji pekee wa kikosi cha Argentina ambaye hakupata kutambuliwa na klabu yake."

"Hiyo ilikuwa inaeleweka ... kwa sababu, kutokana na sisi [Argentina], Ufaransa hawakuhifadhi Kombe la Dunia.”

Rais Nasser Al Khelaifi amekiambia kituo cha habari za spoti cha Ufaransa RMC Sport: "Kama kila mtu alivyoona, na hata tulichapisha video, tulimsherehekea Messi katika uwanja wetu wa mazoezi, na pia tulisherehekea kando.

"Lakini ni muhimu tuzingatie heshima, kwa kuwa sisi ni klabu ya Ufaransa. Kwa kweli ilikuwa hatari kusherehekea kwenye uwanja. Lazima tuheshimu nchi aliowashinda, wachezaji wenzake katika timu ya Ufaransa, na mashabiki wetu wa PSG pia.”

Kauli za rais wa PSG ni kama ilivyoonekana kwenye video iliyochapishwa na PSG mnamo Januari, Messi akifanyiwa gwaride la heshima na wachezaji na wafanyakazi aliporejea kwenye mazoezi na kilabu hiyo ya Parc des Princes.

Hata hivyo mshindi huyo wa Ballon D'or mara saba baadaye aliihama PSG na kuondoka bara Ulaya huku akisainiwa na klabu ya Kimarekani ya Inter Miami.

TRT Afrika