Nahodha wa Argentina Lionel Messi amepokea tuzo ya mwanasoka bora Ulaya Ballon d'Or katika sherehe iliyofanyika ukumbi wa Theatre du Chatelet, ulioko Paris, nchini Ufaransa siku Jumatatu.
Ubingwa huo umemfanya Messi, mwenye umri wa miaka 36, kushinda Ballon d'Or yake ya nane na kuwa na tuzo tatu mbele ya mpinzani wake wa zamani Cristiano Ronaldo, ya tangu aliposhinda Ballon d'Or yake ya kwanza mnamo 2009.
Messi amesema kuwa alitoa ushindi huo kwa heshima ya gwiji wa soka kutoka Aregentina Diego Maradona, ambaye angesherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 63 hapo Jumatatu.
Kwa Messi, kombe hilo linamzawadia, zaidi ya yote, uchezaji wake wa kutia moyo katika Kombe la Dunia mwaka jana, alipoipiga jeki Argentina hadi kushinda, akifunga mabao saba na kutangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo nchini Qatar.
Ilikuwa mara ya kwanza kurejea katika mji mkuu wa Ufaransa baada ya kuondoka Paris Saint-Germain mnamo Juni na kuhamia Inter Miami katika Ligi kuu ya soka nchini Marekani.
"Hii ni zawadi kwa kikosi nzima ya Argentina kwa kile tulichofanikisha," alisema Messi akiwa jukwaani baada ya kupokea tuzo yake kutoka kwa David Beckham, mmiliki mwenza wa Inter Miami.
"Heri ya kuzaliwa Diego. Hii ni kwa ajili yako," alisema.
Messi amenufaika pakubwa kutokana na mabadiliko ya hivi majuzi, kumaanisha kuwa tuzo hiyo inatokana na rekodi ya mchezaji katika msimu uliopita, badala ya mwaka wa kalenda.
"Sikuweza kufikiria kuwa na taaluma niliokuwa nayo. Mafanikio yote niliokuwa nayo. Bahati nimekuwa nayo kuchezea timu bora zaidi duniani, timu bora katika historia. Ni vizuri kushinda mataji haya ya kibinafsi. Kushinda Copa America na kisha Kombe la Dunia, kulikamilisha ni jambo la kushangaza."
Messi alimpiku mshamulizi wa Norway Erling Haaland licha ya kushinda mataji manne katika msimu wake wa kwanza na Manchester City, pamoja na kuvunja rekodi ya kufunga mabao kwenye Ligi kuu ya England.
Haaland aliifungia Manchester City mabao 52 na kufanikiwa kuwa mchezaji bora wa timu.
Aidha, nyota wa Real Madrid, Jude Bellingham alishinda tuzo ya Kopa kwa mchezaji bora wa msimu uliopita mwenye chini ya miaka 21.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 20 ameanza safari yake ya soka Madrid akiwa na mabao 13 katika mechi 13, ingawa amezawadiwa tuzo hiyo kwa uchezaji wake katika kampeni yake ya mwisho akiwa na Wajerumani Borussia Dortmund.
Wachezaji walivyoorodheshwa tuzo za Ballon D'Or
- 1.Lionel Messi
- 2. Erling Haaland
- 3. Kylian Mbappe
- 4. Kevin De Bruyne
- 5. Rodri
- 6. Vinicius
- 7. Julian Alvarez
- 8. Victor Osimhen
- 9. Bernardo Silva
- 10. Luka Modric
- 11. Mohamed Salah
- 12. Robert Lewandowski
- 13. Yassine Bounou
- 14. Ilkay Gundogan
- 15. Emiliano Martinez
- 16. Karim Benzema
- 17. Khvicha Kvaratskhelia
- 18. Jude Bellingham
- 19. Harry Kane
- 20. Lautaro Martinez
- 21. Antoine Griezmann
- 22. Kim Min-jae
- 23. Andre Onana
- 24. Bukayo Saka
- 25. Josko Gvardiol
- 26. Jamal Musiala
- 27. Nicolo Barella
- 28. Randal Kolo Muani
- 29. Martin Odegaard
- 30. Ruben Dias
Tuzo hiyo ya kifahari imetawaliwa na Lionel Messi na mpinzani wake wa jadi Cristiano Ronaldo, kwa miaka 16 sasa huku wawili hao wakishinda kwa jumla ya mara 13 kati yao.