Hatimaye Sherehe ya kila mwaka ya tuzo za soka za ulaya inayosubiriwa sana ya Ballon D'or 2023 itafanyika siku ya jumatatu, tarehe 30 Oktoba kwenye ukumbi wa Theatre du Chatelet ulioko Paris, nchini Ufaransa.
Jumla ya wachezaji 30 wameteuliwa kuwania tuzo hiyo ya mwanasoka bora ulaya, Ballon D'or 2023 wakiwa ni pamoja na Vinícius Júnior, Kylian Mbappé na Kevin De Bruyne huku kila mmoja akiwa na lengo la kushinda au kumaliza katika wachezaji tatu bora bara Ulaya.
Nyota wa zamani wa Chelsea Didier Drogba ndiye atampokeza mshindi tuzo hiyo ya mwanasoka bora ulaya, Ballon D'or 2023, pindi atakapotangazwa siku ya jumatatu.
Tuzo hiyo iliyobebwa na Karim Benzema mwaka uliopita, na kumwezesha kuwa Mfaransa wa kwanza tangu Zinédine Zidane kushinda Ballon D'or, baada ya Kuiongoza Real Madrid kutwaa ligi ya Mabingwa, itakuwa na bingwa mpya mwaka huu.
Nyota wa Argentina na Inter Miami Lionel Messi, ndiye anatabiriwa kushinda Ballon D'or kwa mara ya nane mwaka huu baada ya kushinda Ballon D'or mara saba hapo awali.
Kinachomfanya Messi kutabiriwa kushinda tuzo ya Ballon D'or mwaka huu ni kuwa, nyota huyo alikuwa na msimu usiosahaulika ikiwemo kubeba kombe la Dunia la FIFA 2022 na kuiwezesha Argentina kushinda Kombe lake la tatu la dunia nchini Qatar mnamo Desemba 2022 ambapo alifunga mara saba na kutuzwa mchezaji bora wa mashindano hayo.
Hata hivyo, Erling Haaland anatarajiwa kuwa mshindani mkuu wa Messi, kwani naye amekuwa na kampeni nzuri na klabu yake ya Manchester City katika msimu wa 2022-23.
Haaland alishinda mataji manne katika msimu wake wa kwanza na Manchester City, huku pia akivunja rekodi ya kufunga mabao kwenye Ligi kuu ya uingereza. Haaland alifunga mabao 52 na kutoa pasi 9 za goli kwa Manchester City na kumaliza kama mchezaji bora wa timu.
Tuzo hiyo ya kifahari imetawaliwa na Lionel Messi na mpinzani wake wa jadi Cristiano Ronaldo, kwa miaka 15 huku wawili hao wakishinda kwa jumla ya mara 12 kati yao.
Messi tayari ameshinda Ballon D'or mara saba, mbili zaidi ya mpinzani Cristiano Ronaldo, ambaye ameshinda Ballon D'or tano.