Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio siku ya Jumanne likitangaza Mei 25 kuwa siku ya soka duniani.
Baraza hilo lenye wanachama 193 lilipitisha azimio hilo kwa makubaliano ya kishindo na kukubaliwa na rais wa Baraza, Dennis Francis, ili kuwapongeza wanadiplomasia katika chumba cha mkutano.
Azimio hilo lilifadhiliwa na zaidi ya nchi 160.
Siku hiyo itaadhimisha miaka 100 tangu mashindano ya kwanza ya kimataifa ya soka katika historia na uwakilishi wa maeneo yote ambayo yalifanyika Mei 25, 1924 wakati wa michezo ya Olimpiki ya majira ya Joto iliyofanyika Paris, kulingana na azimio hilo.
Azimio hilo linatambua "kuenea kimataifa kwa mpira wa miguu na mchango wake katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na biashara, amani na diplomasia, na kutambua kwamba mpira wa miguu huunda nafasi ya ushirikiano.”
Pia inatambua "jukumu la msingi" la shirika la kimataifa la soka, FIFA, na jukumu muhimu la mashirika ya soka ya kikanda na kitaifa, pamoja na vyama husika, katika kukuza mchezo.
Azimio hilo linahimiza nchi zote ziunge mkono soka na michezo mengine kama chombo cha kukuza amani, maendeleo na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.
Azimio hilo pia linahimiza nchi kupitisha sera na mipango ya kukuza mpira wa miguu na michezo mingine na afya ya mwili.
Aidha, azimio hilo "linaalika" mataifa yote, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, wasomi, asasi za kiraia na sekta binafsi kuadhimisha siku ya Soka Duniani ifikapo Mei 25, kulingana na vipaumbele vya kitaifa" na kusambaza faida za soka kwa wote, ikiwa ni pamoja na kupitia shughuli za elimu na uhamasishaji wa umma.”