Kipyegon alitetea dhahabu yake kwenye mbio za mita 1500 baada ya kumaliza kwa muda wa 3:54.87. / Picha: AFP

Mwanariadha bora wa kike duniani Faith Kipyegon analenga kuandikisha ushindi mara dufu katika mbio za mita 1500 na 5000 huku fainali ya mbio za wanawake ya mita 5000 ikifanyika leo, mjini Budapest.

Staa huyo, aliyebeba dhahabu kwenye mbio za mita 1500 kwa muda wa 3:54.87, atakuwa uwanjani baadaye katika fainali ya mbio za mita 5000, huku shindano hilo likiwa ni mojawapo ya rekodi tatu za dunia Mkenya huyo asiye na kifani alivunja katika msukosuko wake wa Juni-Julai.

Kufikia sasa, msimu huu Kipyegon tayari ameonyesha kwamba anaweza kuvunja rekodi na pia kushinda medali, akiwa amevunja rekodi za ulimwengu za mita 1500, na 5000 na kushinda dhahabu ya Olimpiki mnamo 2016 na 2022, pamoja na dhahabu ya mashindano ya riadha duniani 2017 na 2022.

Gudaf Tsegay wa Ethiopia, bingwa wa dunia mbio za 10,000m Budapest. Picha: Reuters

Hata hivyo, mbio hizo zinatarajia ushindani mkali huku bingwa mwingine, kutoka Ethiopia Gudaf Tsegay akilenga kutetea taji lake aliloshinda huko Oregon pamoja na kulenga ubingwa wa mara mbili katika mbio za 5000m na 10,000m.

Mkenya mwingine, Beatrice Chebet, ambaye alimaliza wa pili nyuma ya Tsegay kwenye shindano la Diamond League la London pia yuko kwenye kinyang'anyiro hicho.

Aidha, Mholanzi Sifan Hassan, ambaye alianguka katika mbio za mita 10,000 kabla ya kurejea kutwaa medali ya shaba katika kitengo cha mita 1500 nyuma ya Kipyegon, pia ni tishio jingine katika mbio hizo za 5000m.

Mkenya, Emmanuel Wanyonyi ndiye bingwa wa Dunia wa mbio za mita 800 kwa wanariadha chipukizi U-20: Picha: AFP

Mbali na hayo, Mkenya mwingine Emmanuel Wanyoni atakuwa uwanjani kwenye fainali ya mbio za Mita 800 kwa wanaume baadaye leo.

Wanyoni ambaye alimaliza wa nne katika Mashindano ya Dunia yaliyopita huko Oregon mwaka jana, alishinda katika mbio za mchujo na hata nusu fainali mjini Budapest.

TRT Afrika