Timu ya Voliboli ya wanawake ya Kenya maarufu "Malkia Strikers" imeanza kambi ya mazoezi kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa mashindano ya Olimpiki Paris, 2024.
Kikosi hicho kinachofunzwa na Paul Bitok kimewasili mjini Rabat nchini Morocco kwa mafunzo ya mwezi mmoja ya Shirikisho la mpira wa wavu duniani FIVB, ili kuwanoa malkia hao chini ya ukufunzi wa makocha wa kimataifa wakiongozwa na Kocha maarufu kutoka Brazil Luizomar de Moura.
Kenya itaanza safari yake ya kufuzu kwa Olimpiki kwa kuchuana na Colombia kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Challenger ikiwa pia ni pamoja na kusaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mataifa ya Mpira wa Wavu ya FIVB.
Malkia ni mojawapo ya timu zilizofuzu robo fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Challenger pamoja na Colombia, Ufaransa, Mexico, Croatia, Ukraine, Sweden, na Vietnam.
Mashindano hayo ya Challenger yatakayofanyika mjini Laval, Ufaransa yatakuwa muhimu kwa Kenya kwani inahitaji kujizolea pointi za kutosha kupiga jeki harakati zake za kutinga mashindano ya Olimpiki Paris mwakani.
Baada ya kuondoka Ufaransa, Malkia hao wataelekea Yaoundé, Cameroon kushiriki mashindano ya mpira wa wavu kwa wanawake barani Afrika yatakayopigwa kuanzia Agosti mwaka huu.