Kamati ya Utendaji ya shirikisho la soka Afrika CAF ("EXCO") itakutana Mjini Cairo, Misri Jumatano, tarehe 27 Septemba, ili kujadili na kufikia maamuzi yanayohusiana na nchi zitakazopewa haki za kuliandaa Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2027 na AFCON 2025.
Tayari, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro umekutana na Katibu Mkuu wa CAF Véron Mosengo-Omba katika Makao Makuu ya CAF Cairo, Misri huku shughuli ya upigaji kura kuwa mwenyeji wa Afcon 2027 ikisubiriwa kwa hamu.
Tanzania kupitia Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Uganda kupitia (Shirikisho La vyama vya Soka Uganda FUFA, na Kenya ikiwakilishwa na Shirikisho La Soka Kenya FKF ziliwasilisha zabuni ya kwa pamoja maarufu 'AFCON Pamoja' kuandaa makala ya 2027 ya kombe hilo.
Nchi hizo ziliwasilisha zabuni hiyo kwa CAF ndani ya muda uliowekwa wa tarehe 23 Mei 2023.
Aidha Afrika Mashariki inasubiri ushindani mkali wa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kutoka Algeria, Misri na Botswana wanaoshindana kuandaa Kombe hilo.
Mataifa ya Afrika Mashariki na Botswana tu ndio hayajawahi kuyaandaa mashindano hayo kwani Algeria iliandaa Kombe la AFCON mnamo 1990 nayo Misri ilikuwa mwenyeji wa Afcon mwaka 2019.