Waziri wa Michezo Peter Ogwang alikashifu kitendo hicho na kukitaja kuwa cha kutatanisha. 

Kocha wa mchezo wa ndondi nchini Uganda ametiwa mbaroni baada ya kushutumiwa kumpiga viboko bondia wa kike mwenye umri wa miaka 15 kwa kupoteza pambano mwishoni mwa juma katika Ligi ya Mabingwa wa ndondi nchini Uganda, kwa mujibu wa msemaji wa polisi.

Kocha huyo, Herbert Kalungi, alikamatwa na kuhojiwa baada ya video ya tukio hilo kusambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Polisi wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa kimatibabu kwa bondia huyo wa kike kabla ya kuendelea na kesi hiyo, msemaji huyo alisema.

Kikosi cha makocha cha bondia huyo kilirekodiwa kikiwa kimeshikilia mzobemzobe kwa mikono na miguu huku mmoja wao akimpiga mgongoni mara kadhaa.

Kuchochea hasira za wananchi

Watesaji wake walihusisha hasara yake na utovu wa nidhamu, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Video hiyo ilizua taharuki kwa umma na maafisa wa michezo, jambo lililosababisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye pia ni mwanzilishi wa Sparks Boxing Academy.

Naibu msemaji wa Polisi wa Jiji la Kampala Luke Owoyesigyire alisema mwathiriwa na mamake walirekodi taarifa, lakini wamewasihi polisi kutofuatilia suala hilo zaidi kwani linaweza kuhatarisha tamaa yake ya ndondi, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.

Polisi wanasisitiza ni afisi ya mwendesha mashtaka wa umma pekee ndiyo inaweza kufuta kesi hiyo kwani inahusisha mashtaka ya uhalifu uliofanywa dhidi ya mtoto mdogo.

Waziri wa Michezo Peter Ogwang alikashifu kitendo hicho na kukitaja kuwa cha kutatanisha.

"Adhabu ya viboko ni kinyume cha sheria na inaadhibiwa kisheria. Zaidi ya yote, ndondi kama mchezo unasalia kuwa haramu shuleni hadi serikali itakapokuja na kanuni elekezi," alisema katika chapisho kwenye X, ambalo zamani lilijulikana kama Twitter.

TRT Afrika