Vifijo na nderemo zilitikisa uwanja wa mpira wa vikapu wa Kasarani jijini Nairobi, baada ya wenyeji Nairobi City Thunders kunyakua ushindi dhidi ya wageni Uganda City Oilers
Thunders walitwaa ushindi wa 72-62 dhidi ya Waganda na kuweka historia kama timu ya kwanza ya Kenya kufuzu kwa BAL, na kupata ushindi huo mara ya kwanza katika safari ya kwenda BAL.
Wakizungumza baada ya mechi, wachezaji walifurahishwa na mafanikio hayo. Mlinzi wa beki Uchenna Iroegbu, ambaye alijiunga na Thunder mwanzoni mwa mechi zao za kufuzu za Divisheni ya Mashariki alijawa na furaha isiyo kifani.
"Hii inaleta raha sana. Siwezi kuelezea jinsi ninavyohisi, tulifanikiwa mbele ya mashabiki wetu wa nyumbani. Mara ya kwanza katika historia ya Kenya na mara ya kwanza katika historia ya shirika. Nilisema tangu siku ya kwanza kwamba timu hii ilikuwa na uwezo wa kuweka historia. Tulifungwa katika mechi ya kwanza na tumeweka historia usiku wa leo,” alisema mlinzi huyo mwenye asili ya Nigeria, aliyepewa jina la utani la UC.
Thunder wanafuzu kwa BAL 2025, ikiungana na Kriol Star ya Cape Verde ambao pia wanashiriki kwa mara ya kwanza. Waganda Oilers, kwa upande wao, wanakosa kile ambacho kingekuwa kampeni yao ya tatu mfululizo ya BAL.
Kufuatia ushindi huo, Thunder itacheza na Kriol Star katika fainali ya shirikishi lao la Mashariki siku ya Jumanne katika uwanja huo huo - timu zote zikiwa tayari zimefuzu kwa BAL 2025.