Malkia Strikers ilishinda Ubingwa wa Mataifa bora Afrika kwa mara ya mwisho mwaka wa 2015, ikiwa mwandalizi. picha: GETTY

Uhasimu wa Kenya na Cameroon kwenye voliboli unatarajiwa kurejea kwenye uwanja wa michezo wa Yaoundé Jumatano huku pande hizo zikiwania nafasi ya kutua fainali ya dimba hilo.

Kenya ilishuhudia fomu bora kwenye safari yake ya kutinga nusu fainali kufuatia msururu wa kutoshindwa ambapo ilitawala Kundi B, na kushinda mechi zake zote 5 na kuzoa alama 15.

Mchezo huo hautakuwa tu wa kuwania nafasi ya kufika fainali ya michuano hiyo bali pia, ni wa kuwania kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki mwakani jijini Paris, Ufaransa.

Malkia Strikers ya Kenya ambayo ni timu inayoshikilia nambari moja kwenye orodha ya voliboli kwa wanawake duniani, inalenga kukata udhia dhidi ya Cameroon baada ya kupoteza dhidi ya Cameroon huko Yaounde (2017), Cairo (2019) na Kigali (2021) mfululizo.

Kenya ambayo ni moja kati ya timu zilizopigiwa upatu, ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali kumenyana na Cameroon baada ya kuifunga Nigeria 3-0 kwa seti za 25-14,25-17, na 25-12, huku nayo Cameroon ikifika nusu fainali kufuatia ushindi wake dhidi ya Morocco.

Nyota wa Malkia Strikers Veronica Adhiambo ndiye aliibuka mchezaji bora wa mechi kati ya Kenya na Nigeria.

Mshindi kati ya Kenya na Cameroon atakutana na timu itakayoibuka mshindi katika nusu fainali ya pili kati ya Misri na Rwanda, kushindania taji hilo la kuvutia barani.

TRT Afrika