Wazir Khamsin
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Huenda ikawa ni mchezo ambao mzazi alikuwa hodari au mchezo mwingine tofauti kabisa. litia fora enzi zao wakichezea vilabu na wengine hata taifa.Tunaangazia baadhi ya wachezaji ambao walirithi mchezo wa soka kutoka kwa wazazi wao na ndugu zao. Baba zao walitia fora enzi zao wakichezea vilabu na wengine hata taifa.
Divock Origi
Divock Okoth Origi ni mshambuliaji wa timu ya AC Milan iliyoko kwenye ligi ya Italia ya Serie A, amewahi pia kuchezea timu za Liverpool, Wolfsburg na nyinginezo. Amecheza kwenye timu ya taifa ya Ubelgiji.
Ni mtoto wa Mike Okoth ambaye alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya na pia vilabu vya Ubelgiji kama vile KV Oostende na Genk. Divock alizaliwa Ubelgiji wakati baba yake akicheza soka ya kulipwa nchini humo.
Dede na Jordan Ayew
Andre na Jordan Ayew…hawa ni watoto wa mchezaji mwingine nyota aliyevuma enzi zake Abedi Ayew maarufu Abedi Pele. Anatambulika kama mmoja wa wachezaji hodari kuwahi kutoka katika bara la Afrika.
Alikuwa kiungo wa timu ya taifa ya Ghana ambayo aliichezea nchi yake mara 73 na amechezea vilabu katika mataifa mengi ikiwemo Qatar, Uswizi, Benin, Italia na Ufaransa akiwa na timu ya Marseille pamoja na Lyon.
Mwanae Dede Ayew aliyezaliwa Ufaransa yuko kwenye timu ya Le Havre Kaskazini mwa nchi hiyo, naye mdogo wake Dede, Jordan anacheza kwenye timu ya Leicester City inayoshiriki ligi kuu ya England.
Khephren na Marcus Thuram
Jina la Thuram siyo geni kwenye uwanja wa kabumbu. Khephren na Marcus ni watoto wa mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa.
Mchezaji huyo wa safu ya ulinzi alichezea pia vilabu nchini Ufaransa, Uhispania na Italia. Mtoto wa Lilian, Khephren amefuata nyayo za baba yake na yuko kwenye klabu ya Juventus kwenye ligi ya serie A na kaka yake Marcus yuko huko huko nchini Italia na timu ya Inter Milan.
Mbwana Samatta
Mbwana Ally Samatta maarufu kama ‘Kapteni Diego,’ ni mshambuliaji wa timu ya ligi kuu nchini Ugiriki ya PAOK na pia nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars. Amezaliwa kwenye familia ya wachezaji soka.
Baba yake Ally Pazi Samatta aliwahi kucheza kabumbu enzi za ujana wake. Mzee Samatta, aliwarithisha watoto wake kadhaa uhodari huo wa soka, ambapo kaka zake 'Kapteni Diego' wamecheza soka hadi katika ngazi ya ligi kuu ya Tanzania na vilabu mbalimbali.