Mchezaji Nyota wa Tottenham Hotspur kutoka Korea Kusini, Son Heung-min Jumamosi avunja rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kandanda kutoka Asia kufunga mabao 100 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
"Heung-Min Son anakuwa mchezaji wa kwanza kabisa wa Kiasia kufunga mabao 100 kwenye Premier League. Hongera, Sonny," Tottenham Hotspur ilisema kwenye Twitter kumuenzi mshambuliaji wao.
Son, ni mchezaji wa Spurs katika kikosi cha kwanza tangu 2015, alifunga bao lake la 100 la ligi dhidi ya Brighton & Hove Albion katika kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur wa London alipojipinda nje ya eneo na kumpita kipa wa Brighton, Jason Steele.
Kabla ya kujiunga na klabu hiyo ya Uingereza, mchezaji huyo wa kimataifa wa Korea Kusini aliwahi kuzichezea klabu za Ujerumani Hamburg na Bayer Leverkusen.
Tottenham Hotspur iliilaza Brighton kwa bao 2-1, huku mshambuliaji wa Spurs Muingereza Harry Kane akifunga bao la ushindi dakika ya 79.
Spurs inayoshika nafasi ya tano ina pointi 53 katika mechi 30 ili kuzifukuzia Manchester United na Newcastle United, ambazo kwa sasa ziko juu yake zikiwa na pointi 56 kila moja.
Ligi kwa sasa inaongozwa na timu ya Arsenal ambao ndio vinara wakiwa na pointi 72 katika michezo 29, wakifuatiwa na Manchester City wenye pointi 64.