Jurgen Klopp anataka mechi ya Liverpool dhidi ya Tottenham irudiwe kutokana na hitilafu ya VAR iliyowagharimu bao la ufunguzi mwishoni mwa wiki.Picha: Getty

Klabu ya Liverpool inayoshiriki ligi kuu ya Premier nchini England, imesema kuwa suluhu pekee la kumaliza mjadala wa matokeo ya mechi yake dhidi ya Tottenham Hotspurs ni kuchezwa kwa mechi ya marudio kati ya pande hizo.

Spurs ilipata ushindi wa magoli 2 kwa 1 katika mechi hiyo ya ligi kuu na kuvunja rekodi ya Liverpool ya kutofungwa msimu huu.

Liverpool pia waliwapoteza Curtis Jones na Diogo Jota waliolishwa kadi nyekundu.

Waamuzi walikataza kimakosa bao la Luis Diaz kwa sababu ya kutokuelewana juu ya uamuzi wa uwanjani.

Goli la Liverpool lilikataliwa kufuatia kosa la VAR. Picha: Getty

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Klopp alisisitiza kuwa Liverpool haikutendewa haki na hivyo basi kuandikisha matokeo yasiyokuwa sahihi.

"Nimezoea maamuzi mabaya na magumu, lakini kitu kama hiki hakijawahi kutokea na ndio sababu nadhani marudio ndio jambo sahihi la kufanya."

Bodi ya waamuzi katika ligi kuu ya soka England, maarufu (PGMOL) ilitoa sauti iliyonakiliwa kati ya maafisa wa mechi baada ya ombi kutoka Liverpool, lakini bado Klopp anasema kuwa hilo halikubadilisha mawazo yao hata kidogo.

"Sauti iliyotolewa, haikuibadilisha lolote hata kidogo. Ni kosa dhahiri. Nadhani lazima kuwe na suluhisho ya hilo. Nadhani maamuzi yanapaswa kuwa marudio.

PGMOL ilitoa taarifa ikikiri "kosa kubwa la kibinadamu" lilisababisha uamuzi mbaya.

AFP