Marefa wa CAF. Picha CAF

Shirikisho la Soka barani CAF limewateua marefa kutoka Afrika Mashariki kusimamia mechi za Kombe la Mataifa Bora Afrika AFCON, zitakazofanyika Cote D'ivoire 2024.

Marefa hao kutoka Kenya, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan na DRC ni miongoni mwa orodha ya marefa 68 inayojumuisha maafisa wa mechi wenye uzoefu mkubwa barani.

Orodha hiyo ya marefa watakaosimamia mechi hizo ni pamoja na marefa 26, wasaidizi wa wasimamizi 30 na wasimamizi 12 wa VAR ambao wataongoza mechi zilizopangwa kufanyika Cote D'ivoire kati ya tarehe 13 Januari hadi 11 Februari 2024.

Majina ya marefa wakuu wa mechi

  • Ndabihawenimana Pacifique Burundi
  • Weyesa Bamlak Tessema Ethiopia
  • Kamaku Peter Waweru Kenya
  • Ndala Ngambo Jean-Jacques DR Kongo
  • Uwikunda Samuel Rwanda
  • Omar Abdulkadir Artan Somalia
  • Mahmood Ali Mahmood Ismail Sudan

Wakenya Gilbert Cheriyot na Yiembe Stephen wameteuliwa kuwa wasaidizi wa refa kulingana na orodha hiyo iliyo pia na naibu refa kutoka Djibouti Liban Abdoulrazack.

Kwenye mtambo wa VAR, marefa Mukansanga Salima Rhadia kutoka Rwanda na Ibrahim Abdallah Mohamed wa Sudan ndio walioteuliwa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Marefa wote walioteuliwa wanasubiriwa Cote D'ivoire kuanzia tarehe 5 Januari 2024 kwa ajili ya mafunzo zaidi ya ukarabati ambayo yatajumuisha vipimo vya afya na kinadharia wa maafisa wote.

Aidha, kati ya tarehe 11 na 16 Oktoba 2023, marefa walipokea mafunzo ya kuwanoa mjini Abidjan, Cote D'ivoire ili kuhakikisha kuwa maafisa wote walikuwa wanafahamu vyema sheria za soka, VAR na maswala mengine muhimu kwa ubora wa soka barani.

"Uamuzi una jukumu muhimu katika ufanisi wa mashindano, na tunahitaji kuhakikisha kuwa tumejiandaa kikamilifu," mkuu wa CAF wa marefa na teknolojia ya soka, Noumandiez Desire Doue alisema.

TRT Afrika