CBE ya Ethiopia baada ya goli dhidi ya Buja Queens wa Burundi. 

Hatimaye timu nne zitakazoshiriki hatua ya nusu fainali ya mechi za kufuzu kwa kombe la mabingwa CAF barani kwa wanawake unaoendelea chini ya maandalizi ya shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zimejulikana baada ya mechi za makundi kukamilika.

Mechi hizo zote za nusu fainali zitafanyika siku ya jumapili, tarehe 27 jijini Kampala, huku JKT Queens ya Tanzania ikikwatuana na Buja Queens ya Burundi kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza kabla ya wanabenki CBE ya Ethiopia kuvaana na Vihiga Queens kutoka Kenya hapo baadae.

Nusu fainali zitapigwa katika uwanja wa Kituo cha Kiufundi cha shirikisho la soka Uganda, FUFA, Njeru.

Imekuwa ni uchungu kwa mashabiki wa Kampala Queens FC, mwenyeji wa mashindano hayo, baada ya kuchujwa kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kundi A nyuma ya CBE ya Ethiopia na Buja Queens ya Burundi.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Auka Gecheo amesema amefurahishwa na kasi ya ukuaji wa soka la wanawake katika Ukanda huu.

Mshambuliaji wa Kampala Queens FC, Fazila Ikwaput anaongoza jedwali ya wafungaji bora akiwa na mabao nane.

Timu bora zaidi ukanda wa CECAFA itacheza Ligi ya Mabingwa ya CAF ya Wanawake 2023 itakayofanyika Cote d'Ivoire baadae mwaka huu.

TRT Afrika