Uholanzi ilikuwa imetinga robo fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake, lakini kiungo nyota Danielle van de Donk alionekana kutofarijika.
Kadi yake ya njano katika kipindi cha pili cha ushindi wa 2-0 dhidi ya Afrika Kusini Jumapili inamaanisha atatumikia adhabu ya kutocheza mechi moja.
Huenda machozi yake ni kutokana na hofu kuwa anaweza kuwa amecheza mechi yake ya mwisho kombe hili iwapo wataondolewa katika robo fainali dhidi ya Uhispania.
Hata hivyo Kocha wa Uholanzi Andries Jonker alikuwa na mtumaini makubwa zaidi.
"Tumekuja na imani kwamba tunaweza kushinda kila mtu. Na ukisema tunaweza kushinda kila mtu, inajumuisha timu zote, Afrika Kusini, lakini pia Uhispania," alisema.
"Kwa hivyo inamaanisha sio mchezo wa mwisho kwa Danielle. Tunataka kuifunga Uhispania, kisha anaweza kurejea kwenye mashindano."
Kwa hakika Waholanzi wanaonekana kujiimarisha baada ya kushindwa na Marekani katika fainali ya Kombe la Dunia miaka minne iliyopita.
Baada ya kumaliza juu ya Wamarekani katika Kundi E wakati huu, waliishinda Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Soka wa Sydney kupitia mabao ya Jill Roord katika kipindi cha kwanza na Lineth Beerensteyn la pili.
Uhispania ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji, na ilithibitisha dhana hiyo kwa ushindi wa 5-1 dhidi ya Uswizi katika hatua ya 16 bora.
Uholanzi ililazimika kufanya bidii zaidi ili kupata nafasi ya kutinga hatua ya nane bora, huku mlinda mlango Daphne van Domselaar akionyesha uchezaji bora wa mechi kwa kuokoa msururu wa kuokoa Afrika Kusini.
Wenzake walikubali haraka juhudi zake za kuokoa mchezo, wakakimbilia kumkumbatia baada ya filimbi ya mwisho.
"Tulihisi tungeshinda mchezo huu na nikiangalia nyuma, tunapaswa kuwa na nafasi ambazo tulikuwa nazo, lakini hatukuchukua," kocha wa Afrika Kusini Desiree Ellis alisema. "Ukiangalia kipa wao anapata mchezaji bora wa mechi, inakuambia jinsi tulivyocheza vizuri."