Tanzania imefuzu kwa mara ya kwanza tangu 2019. Picha: TFF

Hatimaye washiriki wa michuano ya kumsaka bingwa wa soka barani Afrika, Afcon 2023 nchini Ivory Coast wamethibitishwa, huku orodha ya timu 24 ikibaki tu na nafasi moja.

Jumla ya timu 8 zimejihakikishia nafasi kwenye raundi ya mwisho ya mechi za kufuzu zilizochezwa wikendi hii.

Kutoka kundi A, Nigeria na Guinea Bissau walifuzu huku Sierra Leone na Sao tome na Principe wakiachwa nje ya makala yajayo ya mashindano hayo.

Aidha, Burkina Faso na Cape Verde wamefuzu kutoka Kundi B, huku Togo na Eswatini wakilazimika kubaki pembeni.

Hata hivyo, hakuna timu iliyofuzu kutoka kundi C, kwani, kundi hili lenye timu tatu, limekuwa lenye utata kwani Namibia yenye (pointi 5), Burundi na (pointi 4) na Cameroon yenye (pointi 4) zote zina nafasi sawa ya kufuzu. Aidha, itaamuliwa pale Cameroon na Burundi zitakapokutana tarehe 12 septemba.

Misri, washindi wa medali ya fedha katika toleo la mwisho lililofanyika Cameroon, wamejiunga na Guinea kutua Cote D'ivoire kutoka kundi D huku Malawi na Ethiopia wakilazimika kufuatilia mashindano hayo kwenye runinga.

Kutoka kundi E, Ghana na Angola zimefuzu na kuzipiku Jamhuri ya Afrika ya Kati na Madagascar kufuzu Cote D'ivoire.

Kutoka kundi F, Tanzania na Algeria zilijihakikishia nafasi yao nchini Côte D'ivoire, na kutamatisha Safari ya Uganda na Niger.

Mali na Gambia walihitimu kutoka kundi G huku Kongo na Sudan Kusini zikiondolewa.

Zambia na Côte D'ivoire walihitimu kutoka Kundi H kwani Zambia walihitimu, pamoja na Wenyeji Côte D'ivoire. Comoros na Lesotho wamefunga safari kurudi nyumbani.

Kutoka kundi I, DR Congo na Mauritania walihitimu huku Gabon na Sudan wakiondoka. DR Congo imethibitisha kufuzu kwao baada ya kujipa ushindi muhimu dhidi ya Sudan.

Katika kundi J, Guinea ya Ikweta na Tunisia zimehitimu, na kuwaacha nje Botswana na Libya.

Kundi K, lenye timu tatu, limeshuhudia Afrika Kusini na Morocco kuhitimu, na kuiaga Liberia ikikosa.

Kutoka kundi L, Senegal, mabingwa watetezi wa Afrika, wamehitimu wakiwa na Msumbiji iliyochukua nafasi ya pili kwa kuipiku Benin baada ya kuhitaji tu alama moja ili kufuzu. Rwanda na Benin zimeondolewa kutoka kundi hilo. Imekuwa ni faraja kwa Msumbiji waliofuzu kwa mara ya kwanza tangu 2010.

TRT Afrika