Zikiwa zimesalia chini ya siku 100 kabla ya kombe la mataifa bora Afrika - Afcon 2023 kung'oa nanga nchini Cote D'ivoire, macho yote ya mashabiki wa soka Tanzania na bara la Afrika yameelekezwa kwa kundi F, ambalo limewaleta pamoja Morocco na Tanzania.
Mara ya mwisho pande hizo zilipokutana kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia Brazil 2014, Tanzania iliizaba Morocco 3-1 huku magoli ya Taifa stars yakitiwa kimiani na Mbwana Samatta aliyejinyakulia magoli 2 huku bao jingine likifungwa na Thomas Ulimwengu.
Hata hivyo, hii ni Morocco nyingine ambayo ilifika nusu fainali kombe la dunia Qatar huku pia ikisaka taji lake la pili la Afcon nchini Cote D'ivoire.
"Tuko na kikosi kizuri, kundi zuri na tutajitahidi kushinda, tutajaribu kufanya vizuri wakati huu AFCON, sawa na namna tulivyofanya kwenye kombe la dunia," alisema Hakimi, ambaye pia ni mlinzi wa Paris St-Germain ya Ufaransa baada ya droo huko Abidjan.
Tanzania inalenga kuondoa rekodi ya kutowahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi katika makala yote ya mashindano ya AFCON iliyoshiriki, ikiwemo hivi karibuni mnamo 2019.
Kwa upande wao, wachezaji wa taifa stars ya Tanzania wamefichua kuwa hawana wasiwasi kumenyana na miamba wa soka Afrika katika ngarambe za kombe la taifa bora Afrika Afcon, Cote D'ivoire 2023, huku wakisisitiza kuwa wako tayari "kuwashtua" timu za juu za bara hilo.
"Hakuna majina makubwa tena katika soka. Pengine tunaonekana dhaifu lakini tutapigana kwa bidii tukiwakilisha tumaini la taifa, " amesema Novatus Dismas anayecheza kulipwa Shakhtar, Ukraine.
Kocha wa Morocco, Walid Regragui, ambaye aliiwezesha timu yake kutua nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, ameeleza kutarajia ushindani mkali kwenye kombe la mataifa ya Afrika Cote D'ivoire 2023.
"AFCON ijayo itakuwa ngumu zaidi, na sidhani kuna kundi rahisi, bali usawa," alisema.
Timu mbili bora za kwanza zitafuzu kutoka kila kundi baada mechi za makundi na kutinga hatua ya mtoano, ikiwa ni pamoja na timu nne bora zitakazomaliza katika nafasi ya tatu.
Kombe la Afcon litafanyika kuanzia Januari 13 hadi Februari 11, 2024, katika maeneo sita nchini Ivory Coast ikiwa ni pamoja na kuandaliwa katika viwanja vipya huko Abidjan, Korhogo na San Pedro.
Kundi A: Ivory Coast, Nigeria, Equatorial Guinea, Guinea Bissau
Kundi B: Misri, Ghana, Visiwa vya Cape Verde, Msumbiji
Kundi C: Senegal, Cameroon, Guinea, Gambia
Kundi D: Algeria, Burkina Faso, Mauritania, Angola
Kundi E: Tunisia, Mali, South Africa, Namibia
Kundi F: Morocco, DR Congo, Zambia, Tanzania