Raha ya soka ni ndani ya dakika 90, lakini maandalizi yake ndiyo mapigo ya mchezo huo.
Huku mashabiki wakijawa na matarajio kutokana na furaha isiyozuilika itakayoletwa na msimu ujao wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), utakofanyika Januari 13 hadi Februari 11, 2024, tayari mivutano ya nje ya uwanja imeanza kurindima.
Mashirikisho ya soka ya Kiafrika yamekuwa kwenye msuguano na vilabu vya Ulaya tangu Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kutangaza ratiba ya mashindano, ikiwa na mataifa 24 yaliyojiandaa kupambania kombe katika viwanja sita katika miji mitano ya Côte d'Ivoire.
Vilabu vingi vya Uingereza vinaweza kupoteza wachezaji wao maarufu wa Kiafrika ikiwa AFCON itafanyika katikati ya msimu, na karibu vyote haviko tayari kuwaachilia wachezaji hao kabla ya tukio hilo.
Dk Patrice Mostepe, rais wa CAF, anasisitiza kuwa mashindano hayo yalilazimika kusogezwa kutoka majira ya joto mwezi wa Juni-Julai - yanayoshabihiana na mapumziko ya kimataifa - hadi Januari wakati huu kwa sababu ya hali ya hewa nchini Côte d'Ivoire.
"Si vyema kwa soka la Kiafrika ikiwa tunaweza kuandaa mashindano yanayoweza kufutwa; sio jambo zuri kwa bara zima," Mostepe alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Morocco wakati wa kutangaza ratiba.
Niran Adesanya, mchambuzi na mwandaaji wa michezo wa Nigeria, haonyeshwi kushangazwa na hatua za vilabu vya Ulaya.
"Januari na Februari ni wakati muhimu katika kalenda ya soka. Vilabu vya Magharibi vinarejea kutoka mapumziko ya kimataifa, na kawaida ni wakati bora wa kuijimarisha" Adesanya anaiambia TRT Afrika.
Uchochezi wa moja kwa moja
Mwezi Novemba 2021, kocha wa Liverpool Jürgen Klopp alilazimika kutoa ufafanuzi baada ya kuitaja AFCON kama "mashindano madogo barani Afrika" wakati wa mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
"Mara nyingi nimesikia kwamba hakuna mapumziko ya kimataifa hadi Machi. Januari, kuna mashindano madogo barani Afrika," alisema.
Dhihaka ya Klopp juu ya AFCON iliamsha hisia za hasira kwenye mitandao ya kijamii, na angalau mwandishi mmoja wa Kiafrika kudai kocha huyo aombe msamaha wakati wa mkutano mwingine.
Mjerumani huyo alisema kauli yake ilichukuliwa vibaya, akifafanua kuwa alikuwa tu akionyesha kuchukizwa kwake na kupoteza wachezaji muhimu kama Sadio Mane (Senegal), Mohamed Salah (Misri), na Naby Keita (Guinea) katika mashindano wakati huo.
Mwezi Desemba 2021, wiki chache kabla ya msimu wa Januari 2022 wa mashindano hayo, Rais wa Chama cha Vilabu vya Ulaya, Nasser al-Khelaifi alilalamika juu ya vilabu kupata pigo kwa kutokana na mwingiliano wa kalenda.
Lakini wakati CAF imejitahidi hapo awali, kusogeza mashindano kwa miezi ambayo hali ya hewa sio rafiki kwa soka.
Mafunzo ya Zamani
Katika AFCON 2019, iliyofanyika nchini Misri kati ya Juni na Julai, joto la jua lilikuwa kubwa kiasi kwamba mchezaji wa Uganda Denis Onyango alilazimika kuondolewa uwanjani wakati wa mechi. Mchezaji mwingine alidondoka mazoezini kutokana na kuishiwa maji mwilini.
Ubora wa mashindano hayo haukupata sifa kubwa pia, huku wachambuzi wakitaja kiwango kikubwa cha joto la lilirekodiwa duniani kote wakati huo, hasa maeneo yenye asili ya jangwa, lilidhoofisha uwezo wa wachezaji wakati wa mechi nyingi.
CAF inasisitiza kuwa Januari ni wakati bora wa mwaka kwenye bara hilo kucheza mchezo mzito kama soka. Imekataa kusogea licha ya malalamiko kutoka kwa vilabu vya Ulaya.
"Hapa ndipo wachezaji wanavyochanganyikiwa, hasa wale ambao bado wanachipukia," anasema John Ofori, mchambuzi wa michezo wa Ghana.
"Lakini, kwa bahati mbaya, wanapaswa kuchagua upande. Kucheza kwenye vilabu hivyo ambapo wanavyojipatia kipato na kujenga fani yao. Mara nyingi wachezaji wanajikuta katika nafasi ngumu ya utii."
Mwandaaji wa kipindi cha michezo ya runinga wa Nigeria, Blessing Nwosu anakubaliana. "Hili ni suala kubwa kwa sababu, kama vilabu vya Ulaya vinavyolalamika kwamba wanahitaji wachezaji wao nyota ili kufanya vizuri katika mashindano, vilabu vya Kiafrika pia vinahitaji wachezaji wao nyota kwa kampeni kubwa kama AFCON."
CAF ilifikia makubaliano ya dakika za mwisho na vilabu vya Ulaya kwa AFCON 2022 kuwaachilia wachezaji hadi Januari 3. Ofori anasema makubaliano kama hayo ni kinyume cha uzalendo.
"Ikiwa mashindano ni karibu wiki moja kabla, makocha wanaweza kufanya nini kwa muda mfupi huo? Wachezaji wanaweza kujenga uhusiano wa timu vipi? Wanapata muda gani wa kutengeneza mkakati? Na maana yake ni kuwa sio haki kabisa. Vilabu vya Ulaya vinapaswa kuheshimu mashindano haya zaidi," Ofori anaieleza TRT Afrika.
Vilabu vya Ulaya vimeeleza kwamba wasiwasi wao wa kuwaachilia wachezaji unatokana na hofu ya wachezaji hao kupata majeraha wakati wa AFCON, na hivyo hawataweza kufanya vizuri kwa muda mwingine wa msimu.
Vilabu hivyo pia wanasisitiza kwamba wachezaji wanaoachiliwa wanapata mishahara yao na marupurupu wakati wanacheza kwa nchi zao. Kutokana na sababu hizo ni kwamba vilabu vinastahili kufanya maamuzi makubwa zaidi.
Sheria zinazoegemea Vilabu
Sheria za FIFA hazijasaidia kampeni za timu za soka za Kiafrika. "Vilabu wanapaswa kuwaachilia wachezaji wao waliosajiliwa kwenye timu za kitaifa ambazo mchezaji anastahiki kucheza kulingana na uraia wake ikiwa wito unatoka kwa shirikisho husika," kulingana na kifungu Fulani cha Kanuni.
Lakini sio lazima kwa vilabu kuwaachilia wachezaji nje ya dirisha maalum la kimataifa - hakuna dirisha la Januari - na kwa mashindano makubwa ya kimataifa ya wachezaji wakubwa zaidi ya moja kwa mwaka.
"Ni kama kujaribu kupandisha jiwe kubwa juu ya kilima na viashiria vyote vikiwa kinyume na wewe. Sheria hizo zinapaswa kuifanya iwe lazima kwa vilabu vya Ulaya kuwaachilia wachezaji na kufanya hivyo kwa wakati. Kuifanya kuwa lazima ni sawa na kuomba maamuzi yafanyike kama kibali," anasema Ofori.
Sasa basi, wachezaji wa Kiafrika waliokwama katika hili wanaweza kufanya nini?
"Inategemea sana wachezaji kusimama kidete," anasema Adesanya. "Wachezaji wengi wa Kiafrika wameonyesha njia. Didier Drogba, Michael Essien na Samuel Eto'o, kwa kutaja wachache. Wote waliiambia vilabu vyao, 'Hapana, nitacheza AFCON.'"
Nguvu ya Fedha
Mwezi Agosti 2022, Rais wa Napoli Aurelio De Laurentiis alitangaza kwamba klabu yake haitasaini wachezaji wa Kiafrika isipokuwa wakubaliane kutoshiriki katika AFCON.
Mchezaji wa zamani wa Napoli na Msenegali, Kalidou Koulibaly alikosoa haraka tishio la De Laurentiis, akisema linaweka wachezaji wachanga, wenye vipaji vya Kiafrika wenye njaa ya kujenga kazi na kuishi nje ya nchi, kwenye nafasi ngumu.
"Kwangu mimi, jambo muhimu zaidi ni kuheshimu kila mtu. Huwezi kusema juu ya timu za kitaifa za Kiafrika kwa njia hii. Lazima uwaheshimu, kama vile unavyowaheshimu timu za kitaifa za Ulaya."
Kampeni ya Nigeria katika AFCON 2023 inategemea sana ushiriki wa Osimhen.
Mwanasoka wa Cameroon Eto'o pia alilizungumzia kwa uziyto juu ya suala hilo, akisisitiza kwamba dunia inapaswa kubadilika na ratiba ya mashindano ya kimataifa ya Kiafrika na wachezaji wa Kiafrika lazima wawe kitu kimoja katika utetezi wa AFCON.
Kukosekana kwa mshambuliaji wa Napoli na Nigeria, Victor Osimhen katika michezo ya awali ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 kulikuwa na athari kubwa, na nafasi za Super Eagles kushiriki katika mashindano sasa ziko hatarini.
"Napoli itaweka ugumu kumwachilia Osimhen kwa sababu hawataki ajaribu jeraha kubwa lingine ambalo litamfanya awe nje ya uwanja kwa wiki na kukosa michezo muhimu baada ya AFCON. Lakini basi, fikiria AFCON bila Osimhen kwa mashabiki wa soka wa Nigeria," anasema Nwosu.
Huku mjadala ukiendelea, mashabiki wanaweza tu kutumai kwamba mvutano huu utapata ufumbuzi.
“Sisi tunachotaka ni kwa bara letu kufurahia mchezo wa soka. Tumekupitia changamoto nyingi za kimwili na kiakili. Kama wanadamu nadhani tunastahili kusisimuliwa na furaha itokanayo na mashindano haya” anamalizia Ofori.