Na Agnes Wangari
Ujenzi wa Reli ya Kenya-Uganda unatajwa kwa kuwa kichocheo cha ukuaji ya miji mikuu nchini Kenya kuanzia mwaka1900. Reli hiyo iliyojengwa Waingereza kutoka pwani ya mashariki ya Kenya ya Mombasa hadi magharibi ya nchi huko Kisumu, ilijulikana rasmi kama Reli ya Uganda lakini baadaye ikabatizwa Reli ya Kenya-Uganda.
Maeneo haya yalianza kuvutia uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini ndani ya mikoa na makabila mbalimbali.
Hivyo, lugha ya mawasiliano ilihitajika katika miji na mashamba makubwa yaliyoanzishwa na walowezi wa kikoloni. Mpaka kufikia hatua hii, lugha mchanganyiko kama pijini, ilikuwa imeibuka. Inawezekana kwamba wanajamii wabunifu walianza kutumia hio lugha mseto iliyoibuka katika matumizi anuai na kwa nasibu ikazaliwa lugha ya mtaani inayojulikana kama Sheng.
Sheng, ambayo mara nyingi hudhaniwa kuwa ni msimu uliotokana na Kiswahili-Kiingereza, iliibuka kwa mara ya kwanza katika maeneo yenye mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali jijini Nairobi katika miaka ya 1960. Mbali na Kiingereza na Kiswahili, lugha nyingine za makabila kama Kikuyu, Luyha, Dholuo, na Kikamba pia zimechangia katika lugha hii ya mjini.
Lugha ya Sheng haijatambuliwa rasmi na imejijengea uwezo wa kipekee katika kupokea mabadiliko ya kisarufi. Awali Sheng ilitumiwa kwa mawasiliano baina ya ya watu kutoka maeneo mahsusi. Lakini hivi sasa inabadilika kuwa lugha ya kawaida. Baadhi ya watu waliozaliwa kuanzia miaka ya 1980 na kuendelea, huzungumza Sheng kama lugha yao ya kwanza.
Mfano wa misamiati inajumuisha motii (gari), Muarabe: Mwarabu, na bien (sawa)
Wana-taaluma kutoka maeneo tofauti ulimwenguni wamepata ari ya kutafiti kuhusu Sheng. Takriban miaka kumi iliyopita, utafiti wa kuainisha na kueleza sifa za kiisimu za Sheng ulifanyika. Utafiti ulijumuisha uchambuzi wa kisayansi wa isimu ya Sheng, tathmini ya uainishaji na athari za Shengi kwa jamii ya mijini. Sheng aliwahi kushutumiwa kwa kunajisi lugha "safi" kama vile Kiingereza, Kiswahili, na lugha nyingine za Kenya, na vilevile ilidaiwa kuwa inawaathiri watoto wanaosoma Kiswahili shuleni.
Hata hivyo hali imebadilika sasa. Sheng inasifiwa kuwa inavunja misingi ya kikabila na kuunda sehemu ya kitambulisho cha kitaifa cha lugha. Inawekwa kwenye daraja la Kiswahili cha kikabila au lugha ya vijana. Ingawa tafiti za awali zililenga maeneo mahsusi ya Sheng, neno Sheng kwa sasa linatumika kurejelea aina zote za lugha za mtaani jijini Nairobi ambazo zimeibuka kutokana na Kiswahili.
Kuna mtazamo tofauti kuhusu lugha ya Sheng. Watu wanaoipenda Sheng wanadai kuwa ni kiungo cha mazungumzo ya vijana kwa sababu inaondoa vikwazo vya kibaguzi. Wapinzani wa Sheng wanalalamikia kutoweka kwa lugha sanifu, ugumu wa kuielewa kama sio mjuzi wake, na athari zake kitaaluma. Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kati ya tabia halisi ya kiisimu na matumizi.
Baadhi ya watu, hasa katika maeneo ya vitongoji duni jijini Nairobi, hupuuzia lugha hii katika matumizi yao ya kitaaluma na kuipa thamani kwa kutumia Sheng katika shughuli za kila siku. Watu wengine huwafundisha Sheng watoto wao kama lugha ya kwanza.
Kimsingi, Sheng haijabadilika sana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Jambo lingine la muhimu pia ni kukua na kuenea kwa Sheng katika jamii yote ya Kenya licha ya mitazamo hasi isiyofaa juu ya lugha hii (ambayo imeshindwa kuiathiri).
Sheng inaenea nje ya Kenya kupitia idadi kubwa ya raia wa Kenya waishio nje ya nchi. Sasa hivi kuna kuna ongezeko la tovuti za Sheng ambazo huunganishwa na lugha ya Kiswahili kwa ujumla.
Agnes Wangari ni mhadhiri wa muda wa Historia na Lugha katika Chuo Kikuu cha Strathmore nchini Kenya