Na Ongama Mtimka
Donald Trump na Elon Musk wamejaribu kutikisa muelekeo wa siasa nchini Afrika Kusini wakati taifa likijaribu kuendelea na mipango ya kuwepo kwa amani, uthabiti na umoja kati ya raia wenye asili ya Kiafrika na wazungu kwa lengo la kusawazisha matatizo ya kihistoria.
Utawala wa Trump umeibua madai yasiyokuwa na msingi kuilaumu serikali ya Afrika Kusini kwa kuwalenga wakulima wa kizungu kwa njia isiyo sawa.
Kwa kufanya hivyo amewapa matumaini ya uongo baadhi ya makundi yanayoamini yanaweza kupata matokeo tofauti ya kisiasa wanayoyataka wao licha ya kuwa masuala kama hayo nchini Afrika Kusini hutegemea matokeo ya uchaguzi.
Mara kwa mara makundi hayo ya harakati, yamekuwa yakizusha hofu ili wajinufaishe kisiasa, na pale wanapopata fursa ya kutibua mazingira tulivu.
Wanadhani wanaweza kuitikisa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya demokrasia huku Marekani ikiwapa matumaini ya kuweka shinikizo hilo.
Hata hivyo, hatua yao hii haijafanikiwa, huku watu wa rangi mbali mbali – wengine ambao huikosoa serikali ya Afrika Kusini – sasa wakiitetea serikali dhidi ya kile wanachoona kuwa kuingiliwa kwa uhuru wa taifa lao na Trump na Musk.
Katika mitandao ya kijamii na vyombo vikubwa vya habari kumekuwa na wachambuzi, raia na wanasiasa wanaokabiliana na kampeni za Trump kwenye mitandao hiyo zinazoegemea upande mmoja, anayeonekana kuwakingia kifua Elon Musk na Benjamin Netanyahu.
Musk amekasirika kutokana na serikali ya Afrika Kusini kuitaka kampuni yake ya Starlink ifuate masharti ya mpango wa kuimarisha hali ya uchumi ya watu wenye asili ya Afrika kabla ya uwekezaji wake kuidhinishwa.
Kwa upande wake, Netanyahu ana hasira kuhusu kesi ilowasilishwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai na Afrika Kusini dhidi ya Israeli kuhusu mauaji ya halaiki.
Afrika Kusini imefanikiwa kuangazia kwa makini na kutambua kuwa njama ya Marekani haihusiani kwa vyovyote na maslahi ya wakulima wa kizungu, ambao wanaishi maisha mazuri na ya kifahari katika majumba yao ya ufukweni.
Hawawezi kuhamia Marekani, waache utajiri wao wote nchini humo.
Licha ya wao kuwa 8% ya idadi ya raia wa Afrika Kusini zaidi ya milioni 63, Wazungu ndiyo wenye maisha mazuri zaidi katika taifa hilo.
Mbali na hayo, Afrika Kusini ni moja kati ya nchi chache duniani zenye raia ambao asili ya mababu zao ni walowezi Wazungu, ambazo serikali zao zilihusika katika kuwaondoa katika makazi yao watu wa jamii moja, maujai ya halaiki na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na bado wanatambuliwa kama raia wenye haki sawa baada licha ya utawala wa kisiasa kushikiliwa na wenye asili ya Kiafrika na walio wengi kwenye nchi hiyo.
Na kwa hilo, wako nyumbani nchini Afrika Kusini, taifa ambalo wengi wao wamekuwa wenyeji tangu miaka ya katikati mwa 1600 kipindi ukoloni ulipoanza katika nchi hiyo.
Kwingineko barani Afrika, idadi ya watu wenye asili ya kizungun ilipungua baada ya kupata uhuru, huku Waafrika walio wengi wakichukuwa madaraka wakiongozwa na viongozi wao wakombozi dhidi ya ukoloni.
Mabadiliko ya Afrika Kusini mwanzoni mwa miaka 90 yalitajwa kuwa muujiza. Uchaguzi wa kidemokrasia ambapo kweli kila mtu alipata haki ya kupiga kura 1994, katiba mpya iliyoaminiwa kuwa bora zaidi duniani ilipoanzishwa 1996, na tangu wakati huo nchi imekuwa na uchaguzi wa amani, huru na wa haki.
Sifa ya msingi kwa katiba ya Afrika Kusini, kama inavyoonekana kwenye utangulizi, ni kutambua haki sawa ya kila raia, umiliki wa mali, na uhitaji wa serikali kufanya kila iwezalo kurekebisha hali ya ukandamizaji iliyokuwepo zamani.
Katiba inataka nchi izingatie fursa sawa kwa raia wote na kuhakikisha raslimali zinagawanywa kwa njia inayofaa.
Kipindi chote cha demokrasia, mahakama za nchi zimekuwa mhimili muhimu wa demokrasi yenyewe, zikisifiwa kwa kutatuwa keshi za kisiasa zilizowasilishwa kwao dhidi ya serikali kwa njia ya haki.
Serikali imepoteza kesi nyingi zilowasilishwa mahakamani kutoka mahakama za chini hadi mahakama ya rufaa na mahakama ya kikatiba.
Raia, vyama vya upinzani, makundi mbali mbali, na wafanyabiashara wamefanikiwa kuwasilisha kesi dhidi ya serikali na kushinda katika maeneo ambayo hoja zao zilikuwa na nguvu kuliko zile za serikali.
Mahakama zina utaratibu wa kujilinda dhidi ya uwezo wa mihimili ya serikali na bunge, kiasi cha kuwaghabisha wanasiasa waandamizi wa chama tawala, waliodhani vyama vya upinzani vinatawala nchi kupitia mahakama.
Kwa mfumo wa demokrasia ya kweli, chama cha walio wengi kilitunga sheria na utaratibu kikidhani kitawasaidia kuimarisha siasa na uchumi wa nchi huku nao upinzani wakalazimika kutumia mahakama kupata haki zao pale inapohusisha masuala ya kikatiba. Huo ndiyo umekuwa usawa katika siasa za Afrika Kusini.
Na kutokana na jambo hilo, Rais Cyril Ramaphosa amekuwa na msimamo mzuri akisema kuwa Marekani inajaribu kuishinikiza Afrika Kusini ili iachane na sheria yake kuhusu umiliki wa ardhi na kesi kuhusu mauaji ya halaiki dhidi ya Israeli na kwamba hilo halitofanikiwa na Afrika Kusini ‘’haitokubali kutishwa”.
Mwandishi, Dkt. Ongama Mtimka, ni mchambuzi huru wa masuala ya siasa nchini Afrika Kusini.