Wakuu wa nchi za BRICS./Picha:Reuters

Na Nadim Siraj

Huku mwaka 2024 ukielekea kufika mwisho, kukuwa kwa muungano wa BRICS nchi zinazoimarika kiuchumi ni moja kati ya mafanikio makubwa ya mwaka katika siasa za dunia.

Kwa njia isiyo rasmi BRICS wamekuwa na mchango katika siasa za dunia tangu katikati mwa miaka ya 2000. Lakini mwaka huu, muungano huo ulikuwa na mafanikio zaidi, ukiahidi kuwepo kwa usawa wa uwezo na ushawishi duniani.

Haya yalikuwa matokeo ya kukuwa kwa kasi kwa uwanachama wa muungano huo, kwa kuzingatia ushirikiano, na kuungwa mkono duniani.

Mafanikio ya BRICS ya mwaka huu, yamekuwa kwa kasi kiasi ya kufunika udhibiti wa siasa za dunia uliyokuwa unashikiliwa na kundi linaloongozwa na Marekani la G7.

Kwa wale ambao walikosa taarifa za mabadiliko hayo yaliyofunikwa kutokana na matukio mengine – Gaza, Ukraine, uchaguzi wa Marekani, na Syria – mwaka 2024 ni muhimu sana kwa BRICS.

Matukio kote duniani yanaonyesha kuwa mitazamo yanabadilika yakiangazia usawa wa siasa duniani. Na mwaka 2024 huenda ukawa ni kikomo kwa mataifa machache ya magharibi yanayoongozwa na Marekani ambayo yamekuwa yakiendeleza ubabe.

Ikawa fursa ya kuweka msingi wa siasa za dunia zinazozingatia uwazi, usawa na haki zikiongozwa kidemokrasia na Brazil, Urusi, India, China, Afrika Kusini – mataifa waanzilishi wa BRICS – pamoja na nchini wanachama na mataifa washirika.

Ari ya kujiunga na BRICS

Kwa kutazama matukio yanaonyesha kwa nini mwaka 2024 ulikuwa muhimu kwa siasa za dunia.

Tarehe 1 Januari, mataifa mengine manne, Misri, Falme za Kiarabu, Iran, na Ethiopia – yanajiunga rasmi na BRICS, na kuongeza idadi ya wanachama kutoka watano hadi tisa.

Halafu mwezi Oktoba ikawa hatua nyingine muhimu zaidi wakati muungano huo wa BRICS ulipoalika nchi kumi na mbili kujiunga nao kama ‘mataifa washirika’ – Algeria, Belarus, Bolivia, Cuba, Indonesia, Kazakhstan, Malaysia, Nigeria, Thailand, Uganda, Uzbekistan, na Vietnam.

Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano wa 16 wa BRICS huko Kazan,Urusi, ambao ulihudhuriwa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

Uturuki – ambayo ni mwanachama muhimu wa shirika la NATO – pia walipewa hadhi ya mwanachama mshirika wa BRICS, huku Erdogan akisema kuimarisha ushirikiano na muungano wa BRICS siyo njia mbadala ya makubaliano waliyonayo kama wanachama wa NATO au taifa ambalo liko mbioni kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Akithibitisha kuhusu ombi hilo katikati ya mwezi Novemba, Waziri wa Biashara wa Uturuki Omer Bolat alisema, “Kuhusu hadhi ya Uturuki ndani ya uanachama wa [BRICS], walitupa hadhi ya mwanachama mshirika . Hadhi [hii] ni mchakato wa mpito katika muundo mzima wa BRICS.”

Bila shaka, mataifa mengi yalitaka kujiunga na BRICS mwaka huu, wengine kama wanachama kamili na wengine kama wanachama washirika.

Pamoja na hayo, kulikuwa na taarifa kuwa nchi zisizopungua 40 ziliomba kujiunga na muungao huo.

Ujumbe kwa mataifa ya Magharibi

Kuimarika kwa muungano wa BRICS kumeendelea. Matukio mawili ya hivi karibuni ni ishara ya namna muungano huo ulivyojipanga kuleta mabadiliko chanya duniani ambapo mfumo wa kibabe wa mataifa ya magharibi unaoongozwa na Marekani unapungua.

Moja ni hatua muhimu ya kuanzisha utumiaji wa sarafu mbadala wa dola ya Marekani duniani. Nyingine ni msukumo wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha teknolojia ya AI zaidi ya uwezo wa mataifa ya Magharibi.

Wakati wa mkutano wa mwaka 2024 wa BRICS mjini Kazan, viongozi hao walizindua mfano wa ‘sarafu ya noti ya BRICS’.

Bendera za wanachama waanzilishi wa muungano wa BRICS zimo kwenye noti hiyo. Licha ya kuwa sarafu hiyo haitumiki, uzinduzi huu ni ishara ya mipango ya BRICS kuwa na mbadala wa dola, jambo ambalo mara nyingi linaonekana kama njia ambayo Marekani hutumia kudhibiti uchumi wa dunia.

Pamoja na kuwa bado ni mapema kuhusu suala la kuwa na sarafu ya BRICS, wazo hili linaonyesha nia ya mataifa wanachama kutafuta njia ya kuondoa udhibiti wa dola ya Marekani.

Huku kukiwa na mjadala kuhusu ‘kupunguza matumizi ya dola ’ katika biashara za kimataifa, uzinduzi wa noti ya BRICS uliwashtua kundi la G7.

Hasa baada ya tarehe 23 Oktoba, wakati muungano wa BRICS ulipoidhinisha rasmi malipo kati ya mataifa mbali mbali yafanywe kwa sarafu ya nchi hizo. Muungano huo unataka kuanzisha mfumo wa uchumi ambao hautakuwa ukitegemea ule wa fedha wa Marekani kama SWIFT, mfumo ambao hutumika na mataifa ya Magharibi.

Matukio mengine ambayo haikuwafurahisha wanachama wa kundi la G7 yalitokea tarehe 11 Disemba.

Wakati akihudhuria mkutano wa masuala ya teknolojia ya AI jijini Moscow, Putin alisema Urusi itashirikiana na muungano wa BRICS na mataifa mengine kuimarisha AI. Lengo ni kuunda mbadala wa mfumo wa Marekani ambao wanajaribu kuwa na ushawishi mkubwa kwenye teknolojia hiyo.

G7 vs. BRICS: Mabadiliko ya uhakika

Huku muungano wa BRICS ukiendelea kuimarika kote duniani, swali kuu ni – hii inamaanisha nini kwa kundi la G7 kupoteza ushawishi kwa BRICS?

Mabadiliko ya uhakika ni habari za kusikitisha kwa kundi la G7 kama ilivyo taarifa njema kwa muungano wa BRICS.

G7, au kundi la mataifa saba , ni kundi la mataifa saba yanayojiita yenye uchumi ulioimarika, ikijumuisha Marekani, Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, na Italia. Pia inajumuisha Umoja wa Ulaya, kundi la kiuchumi la mataifa ya Ulaya 27.

Wakiongozwa na Marekani, kwa miaka mingi kundi la G7 limekuwa likielekeza masuala ya ushirikiano wa kimataifa, uchumi wa dunia, na misimamo ya vyombo vya habari na kutotambua michango ya mataifa mengine duniani kama vile China, Urusi, Uturuki na India.

Kuna mabadiliko katika suala la ushawishi na uwezo duniani. Kundi la G7 linapoteza kasi na uwezo – jambo ambalo lisingetarajiwa muongo mmoja uliopita. Mwaka 1990, mataifa ya G7 yalikuwa na jumla ya pato la taifa GDP duniani la asilimia 66 percent na ikawa juu kwa miaka kadhaa.

Wakati huo, mataifa ya Magharibi yanayoongozwa na Marekani yangeamua kuanzisha vita yakitaka, kujiingiza katika katika masuala ya ndani ya nchi zisizoegemea upande wowote, na kupeleka wawakilishi wa Benki ya Dunia na IMF katika nchi maskini.

Mambo yamebadilika sasa. Mwaka 2022, pato la jumla la taifa kwa mataifa ya kundi la G7 limeshuka hadi asilimia 44.

Ukiangalia kwa makini tangu vikosi vya Marekani vilipoondoka Afghanistan mwaka 2021, Marekani haijaanzisha vita vingine vipya. Haijaweza kutatua mizozo na vurugu kwa njia ya amani nchini Ukraine, Gaza, Syria na Yemen.

Kwa nini BRICS ni tofauti

Tofauti yake ni kuwa, pato la taifa kwa mataifa ya BRICS duniani limeapanda hadi asilimia 37. Na licha ya kuongezeka kwa udhibiti wao wa uchumi duniani, muungano huo haujaonyesha nia ya kuanzisha vita vyovyote au kuingilia kati masuala yan chi zingine.

Hili linawezekana kwa sababu muungano wa BRICS unajumuisha mataifa yenye mifumo tofauti ya serikali na mitazamo mbali mbali ya siasa za dunia na sera za kigeni ambazo hazipendi vita, yakilinganishwa na mataifa ya G7 yanayoendekeza ubabe.

Tunapoingia mwaka 2025, G7 ina maswali mengi ya kujiuliza. Muungano wa BRICS, ambao sasa unafahamika kama BRICS + kufwatia kuimarika kwake, ni mataifa yenye jumla ya asilimia 40 ya idadi ya watu duniani.

Mataifa yake yana maliasili nyingi ambayo kundi la G7 haliwezi kuwapuuza. Na muungano huo una uwezo wa kupata soko kubwa la wateja ambalo makampuni makubwa kutoka mataifa ya G7 yanalitegemea.

Huku matukio ya vita vya Ukraine, mapigano ya Gaza, ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi, na vurugu nchini Syria yakiendelea kuenea kwenye vichwa vya habari, kukuwa kimya kimya kwa BRICS bila shaka ni ishara ya moja ya taarifa muhimu na yenye tija mwaka huu.

Imeandikwa na Nadim Siraj, mwandishi wa habari nchini India na mwandishi anayeandika kuhusu masuala ya diplomasia, mizozo na masuala ya kimataifa

TRT Afrika