Ilifungua njia kwa kizazi cha wanasoka wa Kiafrika wenye vipaji waliokwepa mashindano mengine na kukimbilia Uturuki ambapo waliacha historia yao katika Ligi Kuu (Super Lig).
Mbali na Musisi, Wanigeria Daniel Amokachi (Bésiktas), Jay Jay Okocha na Uche Okechukwu; Mmisri Ahmed Hassan (Besiktas); Mghana Stephen Appiah (Fenerbahçe) na Mwafrika Kusini John Leshiba Moshoeu (Fenerbahçe) ni baadhi ya waanzilishi wa wimbi kubwa la Waafrika linaloendelea kupamba Super Lig.
Msimu huu mpya wa soka ulijumuisha takriban wanasoka 60 wa Kiafrika wanaochezea vilabu vya Uturuki. Wanatoka katika nchi mbalimbali barani kote kama vile Senegal, Cameroon, Nigeria, Ghana, Tanzania, DRC, Ivory Coast, Mali, Guinea, Angola, Algeria na Kongo.
Idadi yao huongezeka karibu kila mwaka, kutokana na uimara wa Super Lig, mishahara ya kuvutia, mfumo wa kodi, ubora wa miundombinu na ushabiki tofauti.
Mhamo toka barani Afrika
Vilabu vingi vinaendeshwa na wafanyabiashara na hufurahia na kuvuna mapato zaidi na kupitia hakimiliki za kuonyesha mpira katika televisheni, uuzaji wa hatimiliki, mapato ya filamu na ada za uhamisho.
Mwendelezo wa mtindo huu unawezesha vilabu vya Uturuki kutoa mishahara minono kwa wachezaji wa kigeni, anaelezea mlinzi wa Cameroon Dany Nounkeu, ambaye aliichezea Karabükspor.
Shauku ya mashabiki katika viwanja vilivyojaa pia ni nyenzo muhimu. Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Senegal Ricardo Faty anafahamu vyema michuano ya Uturuki na anaamini kuwa watu wa Uturuki wanaishi na kupumua soka.
“Hapa washabiki wakienda uwanjani hawaendi kutazama kama shoo. Wao ni sehemu ya onyesho!" anaiambia TRT Afrika.
Kakake Ricardo, Jacques, ambaye aliichezea Lazio ya Roma na pia kukaa miaka kadhaa Uturuki, anaamini kwamba mashabiki wa Uturuki “huingia mchezoni" mara zote kama timu wanayoshabikia.
“Wanajua wanaweza kumshawishi mwamuzi, kumkosesha utulivu mpinzani...Kwa kweli wanakuja wamejipanga kucheza na wewe,” anasema.
"Süper Lig kwa kweli ni ligi ya kuvutia. Haiumizi sana kimbinu, lakini ni michuano ya inayovutia kutazama na kutokana na kuwa na wachezaji wengi wanaotoka katika nyanja zote za kiufundi na kimichezo.
Uturuki ni taifa ambalo kila kaya ina klabu inaiyopenda, na hata wale ambao hawafuatilii sana mambo ya soka wanaunga mkono timu fulani. Ilikuwa jambo la kupendeza kucheza huko."
Kwa wachezaji wengi wa Kiafrika wanaotaka kuingia katika duru za klabu za kimataifa, Uturuki pia inaweza kuwa chachu. Wengi wanatumai kung’ara huko na kuvutia vilabu vikubwa vya Ulaya nchini Uingereza, Italia, Uhispania au Ufaransa.
Katika muongo uliopita wa milenia iliyoisha, Musisi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufanya mabadiliko, akijiunga na Bursaspor msimu wa 1994-95 kutoka klabu ya Ufaransa ya Stade Rennais.
Aliacha rekodi nzuri ya kutosha kwa wahusika wengine kutoka Afrika kutulia pamoja na viongozi wa soka wa Uturuki.
Katika miaka ya 2000, kulikuwa na wimbi jingine. Galatasaray ilikuwa mwenyeji wa kikosi hicho cha wachezaji kama Didier Drogba (Ivory Coast), Rigobert Song (Cameroon), Shabani Nonda (Congo), Abdul Kader Keita (Ivory Coast) na Younès Belhanda (Morocco).
Mwakilishi mwingine wa kizazi hiki pia alikuwa Mtogo Emmanuel Adebayor, ambaye alichezea Istanbul Basaksehir, pamoja na Aurélien Chedjou (Cameroon).
Nyota wa zamani wa FC Barcelona na Inter Milan, Samuel Eto'o, anayechukuliwa kuwa gwiji wa si Cameroon pekee bali soka la Afrika kwa ujumla, pia alijitokeza katika michuano ya Uturuki kwa Antalyaspor na Konyaspor. Asamoah Gyan, mfungaji bora katika historia ya soka ya Ghana, pia aliichezea Kayserispor.
Mazingira bora ya kazi
Maamuzi ya wachezaji wa Kiafrika kuendelea kupendelea soka la vilabu vya Uturuki unatokana kwa kiasi kikubwa na kulegezwa masharti vya kusajili wachezaji wa kigeni, vilivyotumika tangu 2015 (14 kwa kila klabu, na uwezekano wa kuchezesha 11 kwa kila mechi), na ongezeko kubwa thamani ya haki za kurusha matangazo ya mechi katika televisheni.
Thamani ya matangazo ilipanda kutoka euro milioni 362 kwa msimu wa 2012-2017 hadi euro milioni 555 kwa msimu wa 2017-2022.
Katika soko la uhamisho wa wachezaji, vilabu vya Uturuki havichezi mbali. Wanatumia mbinu ya kimkakati katika kuvutia wachezaji huku wakiweka msisitizo zaidi katika suala la mishahara.
Yote hii inaungwa mkono na mfumo mzuri wa kodi. Kiwango cha kodi kwa wanasoka ni chini sana kuliko Ufaransa (15% tofauti na 47%). Zaidi ya hayo, tofauti na Ufaransa, ni vilabu vinavyolipa kodi ya wachezaji.
"Tunachopata Ufaransa ni malipo kabla hayajakatwa kodi, hapa tunapata baada ya kodi. Bila kutaja marupurupu mingine, ambayo yanavutia sana," anasema Mkameruni Dany Nounkeu.
Katika suala la usalama, Uturuki imepata maendeleo makubwa. Imetekeleza sera kali sana ya kupambana na ghasia viwanjani.
Ili kufikia hili, mfumo maalum umewekwa, ikiwa ni pamoja na kadi za elektroniki zilizo na taarifa binafsi za wafuasi. "Usalama ndani na karibu na viwanja vya michezo daima uko juu," anasema mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Cameroon Aurélien Chedjou.
Kumiminika kwa Wasenegali
Moussa Sow, Demba Bâ, Papiss Cissé - orodha ya wafungaji bora wa Senegal ambao wamefanya kazi huko Uturuki ni ndefu.
Safari yao ilianza mwaka wa 2002, wakati nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilipofanya kila mtu kuketi na kuwafuatilia kwa makini wakati wa Kombe la Dunia nchini Japan na Korea Kusini. Ongezeko la wachezaji wa Senegal kuingia Uturuki halijakoma tangu wakati huo.
Yote yalianza na maveterani Tony Silva (Trabzonspor, 2008-2010), Diomansy Kamara (Eskişehrspor, 2011 na 2014) na Mamadou Niang (Fenerbahçe SK, 2010, 2011 na Besiktas 2013), na kupelekea kina Desmbas ya Mopisas.
Wa kwanza kati ya wachezaji hao watatu waliotajwa hapo juu alijiunga na Fenerbahçe SK mnamo 2012. Alicheza huko hadi 2015, akifunga mabao 66 katika michezo 154. Alihamia Klabu ya Al-Ahli (UAE), baadaye alitolewa kwa mkopo kwa Fenerbahçe SK wakati wa msimu wa 2016-2017.
Mshambuaji huyo wa Senegal aliendelea kuchezea Bursaspor (2018), Gazişehir Gaziantep FK (2019) na Ümraniyespor (2020-2021).
Demba aliwasili Besiktas mwaka 2014 na kukaa msimu mmoja pekee na klabu hiyo ya Uturuki, lakini ilimtosha kufunga mabao 27 katika michezo 44.
Baadaye alisajiliwa na Göztepe SK kwa msimu mmoja (2018) na kisha kwa İstanbul Başakşehir mnamo 2019, akifunga mabao 26 katika michezo 83.
Papiss aligundua Uturuki kwa kujiunga na Alanyaspor (2018-2020). Alicheza michezo 65 na kufunga mabao 42. Kisha alihamia Fenerbahçe SK (2020-2021) kabla ya kusaini Çaykur Rizespor wakati wa msimu wa 2021-2022.
Kabla ya washambuliaji hawa watatu bora wa Senegal, Issiar Dia alikuwa nyota mwingine aliyesajiliwa na Uturuki. Akianzia soka lake huko Nancy (Ufaransa), alijiunga na Fenerbahçe SK msimu wa 2010-2011 na kufunga mabao 17 katika michezo 48.
Mafanikio ya jumla ya wachezaji hawa wote yanaonekana kuhamasisha watu wengine kutoka nchi yao kuichagua Uturuki kama kitovu chao cha soka kinachowavutia zaidi. Katika msimu huu, kuna angalau wachezaji 10 wa Senegal wanaoshiriki katika ligi ya juu. Kwa furaha ya mashabiki wa Uturuki, nchi yao imesalia kuwa uwanja wa nyota bora wakali kutoka barani Afrika.