Na Elsie Eyakuze
Dhana ya vita kupitia mamluki (proxy war) inazidi kutumiwa zaidi sasa hivi kuliko mwaka wa 2022. Maoni ya Mwanauchumi Jeffrey Sachs yalivuma sana mwezi Machi alipochambua malengo ya Marekani na mfumo wa kisiasa wa China.
Sambamba na hayo, Afrika Kusini iliibua mjadala kidogo iliposhiriki katika mazoezi ya kijeshi pamoja ya wanamaji na Urusi, huku umma ukiunga mkono. Kutoegemea upande wowote kwa China kunaongezeka, India ikiwemo pia, ingawa mara chache sana.
Mazungumzo ninayogusia yote yanatokea miongoni mwa Waafrika, ingawa Vita vya Ukraine haviko mbali sana nasi. Tuko kaskazini kabisa kiasi kwamba baadhi ya watu huweka utani mbaya kwamba tuko salama sana hata ikiwa ugomvi utapelekea matumizi ya mabomu ya nyuklia.
Hili si kweli, lakini linaonyesha wasiwasi fulani kuhusu hatari ya mzozo unaoendelea. Na mazungumzo haya yote yanafanyika kwa sababu Afrika na watu wake wana uzoefu wa kusikitisha wa vita vya kimamluki. Swali la Vita vya Ukraine inamaanisha nini kwetu inaakisi jambo lilelile kwa nini bado tunaijadili zaidi ya Afghanistan, Iran, na pengine hata Kongo.
Linapokuja suala la Mahusiano ya Kimataifa, daima kumekuwa na Afrika mbili. Kuna Afrika ninayoiita nyumbani, yaani eneo kubwa la ardhi lenye muundo tata wa tamaduni, mfumo wa ikolojia, lugha na uzoefu tofauti. Inajumuisha familia, marafiki na mapenzi ya soka na wasiwasi juu ya gharama ya petroli, na maisha ya kila siku. Halafu kuna Afrika ya habari na kiuchumi na "mahusiano ya kimkakati," ambayo hutolewa kwa misingi ya idadi.
Nchi yangu inazungumziwa kulingana na Pato la Taifa kwa kila mtu, amana za tanzanite au dhahabu, ekari ya ardhi ya kilimo, na thamani ya mali isiyohamishika ya ukanda wa pwani. 'rasilimali' ni neno linalotumika. Afrika ina utajiri wa "rasilimali", na penye rasilimali huja maslahi.
Ninaposikia mazungumzo mengi juu ya rasilimali za Kiafrika na neno linaloambatana nayo, "utajiri", bila kusikia juu ya Waafrika wenyewe, msemo unakuja akilini: mataifa hayana marafiki; wana maslahi.
Historia ya Afrika imekuwa kielelezo cha ukweli huu kwa karne nyingi, na chini ya kauli kama ‘Afrika Inaiuka’, nadhani tunafahamu kwamba maslahi bado yanazidisha urafiki na kwamba udhibiti wa rasilimali kwa uwekezaji wa kigeni- au uingiliaji wa kigeni- ni sehemu ya ukweli wa sasa kwa mataifa ambayo utajiri wao umekuwa ukichukuliwa mara kwa mara.
Kwa hivyo mtazamo uliotajwa hapo juu kuhusu Vita vya Ukraine unahusu kuelewa ni maslahi gani ya kuzingatia inapokuja suala la ustawi wa Waafrika. Mahusiano yetu fulani, kama vile kati ya Ulaya na Marekani, yanaeleweka vyema. Hata kama taifa linajiona liko huru katika siasa za leo, ikukumbukwe kwamba, yote hii imetokana na ubeberu wa kale.
China imejidhihirisha kuwa yenyewe inajitanua kwa njia tofauti. Kwa kubadilishana mikopo yenye ukarimu usio wa kawaida, huku wakichukua ardhi na miundombinu muhimu katika nchi, na kudhoofisha uhuru wa mataifa hayo moja kwa moja. Namna China inashughulika na wa maeneo iliyojimilikisha, inatia shaka madai ya ya kutokuwa beberu mpya.
India, ingawa ni mdau muhimu katika maeneo mengi, inaonekana kuridhishwa na uhusiano wa kiuchumi unaotegemea biashara na huduma, usioonyesha kitisho. Wiki hii tu, ilitangaza mikataba ya ufanyaji biashara kupitia Rupia na fedha za mataifa husika kadhaa, na kudhoofisha ukiritimba wa Dola ya Marekani katika uchumi wa dunia.
Katika mwaka 2023 ni dhahiri kuwa kuna kitu kinaendelea katika nyanja za watawala wenye nguvu duniani. Ni dhahiri kwamba ushawishi wa Marekani unapingwa kimya kimya huku zikiibuka nchi nyingine zinazotaka kuwa na sauti.
Hii imewiana na kuongezeka kwa 'Washirika wa Maendeleo' wapya barani Afrika. Mbali na uwekezaji wa China na India, kumekuwa na mtindo wa nchi kutoka Mashariki ya Kati kuwekeza katika mataifa ya Afrika ambako kuna mshikamano unaozingatia dini na utamaduni wa Kiislamu wa pamoja kwa mfano, au kwa biashara tu.
Nchi nyingine za Asia kama vile Japani zinaweza kuwa na mtazamo thabiti kuhusu hali halisi ya mahusiano ya kiuchumi. Fursa hizi bila shaka zinakaribishwa kwani nchi yoyote yenye inayojielewa inajua kuwa mchanganyiko wa fursa mbalimbali za kibiashara ni kitu kizuri. Hata hivyo daima huwa kuna mashaka kidogo pale mahusiano mapya yanapojengwa na hili ni nadra kusemwa hadharani.
Afrika inachukuliwa kuwa bara maskini zaidi na la kusikitisha zaidi duniani inapokuja katika masuala ya siasa za kimataifa huku pia ikiwa na rasilimali nyingi na idadi ya watu vijana wenye nguvu ambayo inakua kwa kasi. Tunafahamu hali hii ya tatizo: kuwa chini ya mstari wa ustawi bora.
Mtazamo kama huo unapelekea vizazi vichanga vya Waafrika kuhofia uhusiano mapya na wa zamani. Kuna ongezeko la nchi, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutaka kulinda maslahi yake binafsi kwa ujumla. Kimsingi, mgawanyiko wa bara la Afrika yaani Kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika ya Sahelian, unaweka bayana baadhi ya changamoto zinazotatiza Umoja wa Afrika.
Katika tukio hilo, tukiangalia uhusiano tata wa mataifa ya Afrika na mataifa mengine ya dunia, itikadi si jambo la muhimu tena. Tunaweza kuema kuwa itikadi za mrengo wa kushoto au wa kulia, huria dhidi ya wahafidhina zilipitishwa tu kama sehemu ya misemo tu ya kimahusiano ya kimataifa. Ni masuala ya juujuu tu yanayotumika lakini kimsingi hayana mizizi katika fikra za Kiafrika. Hivyo, mashinikizo kwamba Afrika ichague upande, hasa katika migogoro ya kiitikadi inaweza kutoa matokeo ya kushangaza. Wakati Afrika inapoichagua Afrika kwanza, dhamira yake inapewa kipaumbele kuliko kaulimbiu za itikadi za na hivyo kuweka maslahi ya Afrika mbele katika dunia ambao ni nadra huwa na ukarimu.
Hili ni jambo ambalo Rais Zelensky wa Ukraine aliligundua kwa maumivu wakati ombi lake la kuwahutubia wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika lilipokataliwa.
Ni dhahiri kuwa nchi za Kiafrika hutumia mbinu ya kawaida ya kutawanya kura au kutopiga kabisa katika maazimio ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Urusi. Afrika inapendelewa mazungumzo niliyorejelea mwanzoni mwa makala.
Linapokuja suala la mielekeo ya kiitikadi, mabadiliko ya kimataifa katika uwezo, migogoro na biashara, Afrika imejifunza baada ya miaka 50 ya Uhuru kwamba tahadhari na maslahi binafsi ndiyo sera pekee zinazotegemewa kwa ushiriki endelevu na wa uhakika.
Elsie Eyakuze ni mwandishi anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Amekuwa mwandishi wa gazeti la The East African kwa zaidi ya muongo mmoja. Pia anachangia kwenye machapisho katika eneo la Masuala ya Afrika.