India TikTok / Photo: AP

TikTok, mtandao maarufu ya kueneza video kwa njia fupi ambao umewageuza wanafunzi na akina mama nyumbani kuwa watu mashuhuri, umekuwa katikati ya utata katika miaka ya hivi karibuni.

Licha ya kujizolea umaarufu miongoni mwa vijana, hata hivyo imekabiliwa na shutuma za ukiukaji wa faragha na wasiwasi juu ya madai yake ya uhusiano na serikali ya China.

Siku ya Jumanne wiki hii, Spika wa Bunge la Kenya Moses Wetangula, alipokea mswada kutoka mlalamishi aliyetaka TikTok ipigwe marufuku nchini Kenya kwa kueneza ngono, lugha isiyokuwa ya kinidhamu, uchochezi, chuki na kuchangia uharibifu wa maadili nchini humo.

India ilikuwa nchi ya kwanza kuipiga marufuku TikTok mnamo Juni 2020, ikitaja wasiwasi juu ya usalama wa kitaifa na faragha ya data.

Hatua hiyo ilionekana kama sehemu ya ukandamizaji mpana dhidi ya mtandao huo na kampuni za China huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

Vikwazo hivyo viliacha kampuni anzilishi ya TikTok, ByteDance, ikiyumba kwani India ilikuwa soko lake kubwa zaidi, ikiwa na watumiaji zaidi ya milioni 200.

Mtumiaji wa TikTok kutoka Italy, mwenye asili ya Senegal, Khaby. Picha: Reuters

Mnamo Julai 2020, Marekani pia ilizingatia kupiga marufuku TikTok, ikitaja wasiwasi juu ya usalama wa kitaifa na faragha ya data.

Utawala uliotangualia wa Trump ulitishia kupiga marufuku Tiktok isipouzwa kwa kampuni moja ya Marekani, ikitaja wasiwasi wake kuwa programu hiyo ina uwezo wa kutumiwa na serikali ya China kuwapeleleza Wamarekani.

Licha ya majaribio ya serikali ya Trump kupiga marufuku programu hiyo, mnamo Septemba 2020, jaji wa wa jimbo alizuia marufuku hiyo, akisema kuwa ilikuwa "ya kiholela na isiyo na maana".

Walakini, licha ya upinzani wa awali, serikali ya Marekani iliidhinisha marufuku ambayo haijawahi kufanywa juu ya utumiaji wa TikTok kwenye vifaa vya serikali ya majimbo mnamo Desemba iliyopita.

Kwa hivyo, zaidi ya nusu ya majimbo ya bunge la Congress yamepiga marufuku TikTok kutoka kwa vifaa rasmi vya serikali.

Marekani, Umoja wa Ulaya, Canada kuchukua hatua

Mnamo mwezi Machi, Ikulu ya White House iliongeza marufuku hiyo kujumuisha mashirika yote ya serikali, na kuwapa wafanyakazi wa serikali siku 30 kuondoa programu kutoka kwa vifaa vyao vya kazi.

Wakati huo huo, tawi kuu la EU lilipiga marufuku TikTok kwa simu zinazotumiwa na wafanyakazi kama hatua ya usalama mtandaoni.

Aidha, mwezi huo huo wa Machi, Bunge la Ulaya lilifuata hatua hiyo, kwa kuwapiga marufuku wafanyakazi kuweka programu kwenye simu yoyote iliyokuwa na uwezo wa kufikia barua pepe au mitandao ya bunge.

Vilevile, Canada ilijiunga na Marekani na Umoja wa Ulaya katika kupiga marufuku, na kuzuia TikTok kusakinishwa kwenye vifaa vyote vya simu ya mkononi vilivyotolewa na serikali, huku maafisa wa Magharibi wakichukua hatua dhidi ya programu ya kushiriki video inayomilikiwa na China.

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, amewataka Wakanada watafakari juu ya usalama wa data zao TikTok. Picha: AP

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, hakuficha uwezekano wa kuchukua hatua zaidi. "Ninashuku kuwa serikali inapochukua hatua muhimu ya kuwaambia wafanyakazi wote wa shirikisho kwamba hawawezi tena kutumia TikTok kwenye simu zao za kazi, Wacanada wengi kutoka kwa biashara hadi watu binafsi nao, watafakari juu ya usalama wa data zao na labda kufanya uamuzi," alisema.

Mnamo Machi 1, serikali ya Uturuki iliitoza TikTok faini ya jumla ya lira milioni 1.75 (dola 93,000) kwa kutochukua hatua za kutosha kulinda watumiaji dhidi ya usindikaji haramu wa data zao, Bodi ya Ulinzi wa Data ya Kibinafsi (KVKK) ilisema.

Msemaji Zabihullah Mujahid. Uongozi wa Taliban Afghanistan ulipiga marufuku TikTok Septemba 2022 ili kuwalinda vijana. Picha: AFP

Nchi kadhaa pia zimechukua hatua dhidi ya TikTok. Mnamo Januari 2021, Pakistan ilipiga marufuku TikTok kwa kueneza maudhui "yasiofaa na machafu", huku mnamo Februari 2021, Myanmar nayo ikiipiga marufuku programu hiyo kama sehemu ya ukandamizaji mkubwa dhidi ya mitandao ya kijamii kufuatia mapinduzi ya kijeshi.

Mnamo Juni 2021, utawala wa Nigeria pia ulipiga marufuku TikTok, ikitaja wasiwasi wake juu ya "matumizi ya jukwaa hilo kwa shughuli ambazo zinaweza kudhoofisha uwepo wa shirika la Nigeria."

Uongozi wa Taliban wa Afghanistan ulipiga marufuku TikTok na mchezo wa PUBG mnamo Septemba 2022 kwa misingi ya kuwalinda vijana dhidi ya "kupotoshwa."

Mnamo Desemba 2022, Taiwan iliweka marufuku ya sekta ya umma kwa TikTok baada ya FBI kuonya kwamba TikTok inahatarisha usalama wa kitaifa.

Marufuku ya TikTok, zua mjadala

Marufuku ya TikTok yamezua mjadala juu ya jukumu la kampuni za mitandao ya kijamii ya kulinda data na faragha ya watumiaji. Baadhi wanahoji kuwa marufuku hayo ni muhimu ili kulinda usalama wa taifa na kuzuia serikali za kigeni kupata taarifa nyeti, huku wengine wakiona marufuku hayo kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa kujieleza.

Licha ya marufuku, TikTok inasalia kuwa mojawapo ya mtandao maarufu zaidi ulimwenguni, ikiwa na zaidi ya watumiaji bilioni moja ulimwenguni.

TikTok imechukua hatua za kushughulikia masuala ya faragha na usalama, ikiwa ni pamoja na kufungua "kituo cha uwazi" nchini Marekani ili kuruhusu wataalamu kutoka nje kukagua sera na mienendo yake.

Yote tisa, marufuku ya TikTok yanaonyesha wasiwasi unaokua juu ya faragha na usalama wa kitaifa katika ulimwengu unaozidi kushikamana.

Ingawa baadhi ya nchi zimechagua kupiga marufuku programu moja kwa moja, zingine zimeweka vizuizi au zimetaka uangalizi mkubwa zaidi wa kampuni za mitandao ya kijamii.

Huku mjadala juu ya nafasi na jukumu la mitandao ya kijamii katika jamii ukiendelea, inabakia kuonekana jinsi serikali na makampuni ya teknolojia yatakavyounda usawa katika maslahi yanayoshindana ya faragha, usalama, na uhuru wa kujieleza.

TRT Afrika na mashirika ya habari