Na Coletta Wanjohi
Akiwa amezama katika mawazo mengi, Esther Gaceke anatembea kuelekea nyumbani kwenye barabara jebamba inayogawanyisha manyumba madogo madogo yaliojengwa kwa mabati.
Maelefu ya watu wanaishi katika eneo hili la makazi duni ya kijiji hiki cha Kibagare, jijini Nairobi, nchini Kenya.
Jua la alasiri ni kali sana hivi kwamba baadhi ya watu wamejificha kwenye vivuli vya maduka madogo madogo kwenye kila upande wa barabara yenye vumbi ya mtaa huo wa mabanda, huku wengine wakiendelea kujifuta jasho wanapofanya biashara zao chini ya jua moja kwa moja.
Esther mwenye umri wa miaka 15 anastahimili joto ndani ya koti ambalo limefungwa zipu kabisa. Bado ana aibu ya ujauzito wake wa miezi mitatu.
"Nipo katika hali ngumu sana kimawazo kwasababu sisi si matajiri nyumbani " anaiambia TRT Afrika.
Nyumbani mama yake amejaa mawazo, amezubaa akiangalia tu mlangoni. Esther anapoingia anainua macho na kumtazama bila kusema lolote na badaye kurudi kuzubaa akiangalia mlangoni.
“Kulala njaa si jambo geni kwangu na kwa ndugu zangu wawili,” Esther anaieleza TRT Afrika huku machozi yakitiririka mashavuni mwake, “siku ambayo ilipelekea nijipate katika hali hii, mama alikuwa akimhudumia baba yetu ambaye alikuwa amelazwa hospitalini.
Siku mbili alikaa huko.
"Mwanamume mmoja aliyekuwa rafiki yangu alinipa pesa za chakula na akanishawishi niende nyumbani kwake.” anaelezea Esther.
Katika kijiji kama hiki cha Kibagare chenye idadi kubwa ya watu wanaoishi karibu karibu hakuna kitu kisichojulikana, na ujauzito wa Esther umekuwa gumzo la hivi punde katika eneo hilo.
Anasema baadhi ya watu huzungumza waziwazi juu yake, baadhi ya wale wa rika yake humcheka na kumdhihaki na kuna watu wengine hasa waliokomaa ambao humkashifu kuwa amekuwa msherati.
"Nimekuwa na ushawishi kutoka kwa marafiki wa kutoa hii mimba au kutoroka nyumbani, lakini nimeanza kujipa moyo na kujiambia kwamba ninaweza kurudi shuleni baada ya kujifungua, " Esther anasema akipanguza machozi.
Na akimwangalia mama yake huku akishindwa kujidhibiti analia kwa sauti,
"Mama, najua nimekukatisha tamaa lakini baada ya miezi 6, nitajifungua mtoto mwenye afya njema, nirudi shuleni na kukufanya ujivunie siku zijazo, tafadhali nivumilie, tafadhali."
Takriban wasichana 330,000 chini ya umri wa miaka kumi na minane hupata mimba kila mwaka nchini Kenya, kulingana na data kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu.
Esther anasema anapenda kazi ya kuoka keki na anataka kusomea mapishi na kufungua maduka ya keki jijini katika siku zijazo.
Mama yake pia hawezi kuficha machozi yake huku akionekana anaamini kile mwanaye amemuahidi.
Kwa sasa anasema anachowaza zaidi ni jinsi atakavyomlea mtoto wa mtoto wake ilhali hata kuwalea wake maana watatu ni changamoto kubwa sana kwasababu ya kukosa hela ya kutosha.
Kuteleza Si Kuanguka
“Hodiii hapa, nani yuko?” sauti inaitana nje na baadaye kufuatwa na binti mwenye tabasamu pana.
Uchangamfu wake unaonekana kuhitajika sana katika nyumba hii ya akina Esther , wanachangamka wanapomwona.
Grace Wambui mwenye umri wa miaka 16 anaketi karibu na Esther, nakumfuta machozi bila kuuliza kwa nini analia, kwasababu alikuwa katika hali hii ya rafiki yake takribani miaka miwili iliyopita.
"Mama Esther, nimekuja kumuaga Esther, narudi shuleni," Wambui anamweleza mamake Esther kisha kumgeukia rafiki yake,
“Usijali Esther, najua jinsi ilivyo ngumu hasa kwa watu wanaozungumza kuhusu wewe sasa kijijini kwetu, lakini usiogope, uwe na nguvu na uendelee kuwa makini kama vile tunavyozungumza kila mara, sawa?” Esther anatabasamu na mara kwa mara wanacheka na Wambui kwa nguvu huku akimsindikiza hadi kando ya barabara.
Anaendelea kupunga mkono huku akimtazama rafiki yake akirudi nyumbani kujiandaa kurudi shule.
Wambui anatembea kwa majivuno. Mara kwa mara anawasalamia watu anaowafahamu njiani, wengine wakimtakia heri anaporejea shuleni na kwa wale ambao wanaonekana hawajui, anahakikisha anawaambia kwamba yeye anarudi shuleni.
Katika mitaa ya kijiji cha Kibagare pilika pilika za watoto kurudi shule iko juu. Watoto kutoka shule tofauti za sekondari wazunguka, wengine wakielekea shuleni huku wengine wakiharakisha kufanya ununuzi wa dakika za mwisho.
Wambui anakutana na baadhi ya wanafunzi wenzake na wanataniana na kucheka kwa sauti, wakikumbushana wafike shuleni kabla ya saa tisa mchana. Anapofika nyumbani anakuta mama yake tayari amemsaidia kupanga mahitaji yake ya shule.
"Nilipogundua binti yangu ni mja mzito, nilivunjika moyo sana kwa sababu mimi ni mtu wa dini na sikuweza kufikiria Wambui angeweza kufanya hivyo, kila mtu katika kijiji hiki anajua nilivyo mkali." mamake Wambui anaiambia TRT Afrika.
"Imenichukuwa muda sana kukubali yaliyojiri lakini nikimwangalia mtoto wa Wambui ananipa furaha .” Mama yake alikuwa mjane miaka sita iliyopita na sasa ndiye mlezi pekee wa watoto sita.
Mtoto wa Wambui mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ni mcheshi sana. Anamtazama mama yake akishughulika na mara kwa mara anacheza naye.
“Nilivutiwa na zawadi na maneno matamu kutoka kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 20,” Wambui anaeleza huku aking’arisha viatu vyake.
"Mama yangu alinipa ushauri mara kwa mara kuhusu jinsi ya kuepuka vishawishi vya wanaume,na nilipopata mimba nikiwa na miaka kumi na nne, wasiwasi wangu ulikuwa, kuwa nimemkosea mama sana na nimeharibu maisha yangu. ”
Wambui alifanya mitihani ya darasa la nane akiwa mjamzito na akafaulu sana. Mwaka mmoja baadaye alipata nafasi katika shule ya sekondari ya bweni iliyopo ndani ya kijiji cha Kibagare, mita chache tu kutoka nyumbani kwao.
“Ninafurahi nilifanya uamuzi wa kurudi shuleni, kuteleza sio kuanguka , nilikosea lakini mtoto wangu ni baraka na motisha yangu maishani. ”
Akiwa shuleni anasema amelazimika kupuuza wasichana wengine ambao humtusi kuwa yeye ni mama shuleni.
Mamake Wambui anaridhika jinsi bintiye anavyoweka bidii shuleni.
"Binti yangu na mwanaye wote ni watoto wachanga " anatabasamu huku akimwangalia bintiye aliyevalia sare za shule , "Wambui anatia bidii sana katika masomo ya sayansi, huwa namwambia akumbuke kwamba lazima afaulu kwa ajili ya mtoto wake.”
Akiwa tayari Wambui anambeba mwanawe kwa muda na kumuahidi kwamba atamrudishia mafanikio.
Mtoto anatabasamu kana kwamba anaelewa.
"Ndoto yangu ni kuwa mhadhiri katika chuo kikuu hapa nchini Kenya, najua nitafanikiwa," anaiambia TRT Afrika huku akimkabidhi mama yake mtoto.
Anapochukua begi lake mama yake anamkumbusha kwamba elimu ndiyo njia pekee ya kutoka katika makazi duni wanapoishi kwa hivyo ni lazima aendelee kufanya bidii.
Wambui anafuta machozi mara kwa mara akigeuka kuwatazama mama yake na mwanaye waliosimama mlangoni kwao wakimtazama akienda shuleni.