Tamasha hilo la kwanza la Giants of Africa, litakuwa pia ni maadhimisho ya ukumbusho wa miaka 20 tangu uanzilishi wa shirika la Giants of Africa/ Picha:  Giants of Africa 

Rais wa Rwanda Paul Kagame na Mama wa taifa Jeannette Kagame ni wenyeji wa vijana kutoka Kenya, Tanzania, Nigeria, Burkina Faso, Ivory Coast, Rwanda, DRC, Senegal, Somalia, Uganda, Botswana, Ghana, Sudan Kusini, Morocco, Cameroon na Mali kwa tamasha kubwa la vijana barani, maarufu Giants of Africa.

Ukumbi wa BK Arena, Kigali, Rwanda. Picha: Reuters

Kulingana na Masai Ujiri, mwanzilishi wa Giants of Africa, shirika lisilo la faida linalojitolea kutajirisha maisha ya vijana wa Kiafrika kupitia michezo, tamasha hilo linalenga kuwaunganisha na kusherehekea kizazi kijacho cha viongozi barani Afrika kupitia mpira wa vikapu, elimu, utamaduni, na burudani.

Kama rais wa Raptors, aliwasaidia kushinda Ubingwa wao wa kwanza wa NBA mnamo 2019. Picha: Raptors

Aidha, vijana hao wapatao 250, walioweka kambi, wataweza kuwasikia viongozi wakuu wa tasnia mbalimbali katika ulimwengu wa michezo, burudani, siasa na biashara watakaozungumzia mada tofauti ikiwa ni pamoja na uongozi, uwezeshaji wa wanawake, kubadilisha mawazo kuwa vitendo, na maendeleo ya kitaaluma.

Zaidi ya vijana 250 kutoka nchi mbali mbali Afrika wamepiga kambi kuhudhuria tamasha hilo Kigali. Picha: Giants of Africa.

Masai Ujiri, ambaye ni Makamu Mwenyekiti na Rais wa Toronto Raptors, alipata umaarufu baada ya kuweka historia kwa kuwa Rais wa kwanza na wa pekee mzaliwa wa Kiafrika kuwa msimamizi wa kampuni ya kitaaluma ya michezo katika maeneo ya Amerika Kaskazini.

Tamasha hilo la kwanza la Giants of Africa, litakuwa pia ni maadhimisho ya ukumbusho wa miaka 20 tangu uanzilishi wa shirika la Giants of Africa, ambalo kuanzia 2021, hadi leo, limejenga viwanja 26 vya mpira wa vikapu nchini Kenya, Tanzania, Nigeria, Burkina Faso, Ivory Coast, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Senegal, na Somalia kupitia mradi liliozindua wa mpango wa 'Kujengwa Ndani' viwanja 100 vya mpira wa vikapu.

Kuanzia 2021 hadi sasa, Giants of Africa imejenga viwanja 26 vya mpira wa vikapu barani Afrika . Picha: AP

Miongoni mwa Nyota wa Mziki watakaoshiriki kwenye tamasha hizo ni pamoja na Diamond Platnumz, Davido, Tiwa Savage, Bruce Melodie, Tyla, na wengineo katika uwanja wa BK Arena, Kigali.

Mashindano ya siku tatu ya mpira wa kikapu kwa wavulana na wasichana wanaowakilisha mataifa yao, pia yameratibiwa ili kuwasaka mabingwa wa tamasha hilo la Giants Of Africa 2023.

TRT Afrika