Msanii wa Tanzani Diamond Platnumz maarufu Simba, amethibitisha kwa mara nyingine kwa nini anasifika kuwa mojawapo ya vipaji na fahari kubwa ya afrika, Afrika Mashariki na Tanzania, baada ya kushinda kwenye tuzo za muziki za MTV Ulaya 2023 (MTVEMA) zilizofanyika Paris kwa mara ya kwanza tangu 1995.
Diamond Platnumz alishinda tuzo hiyo kwa mara ya kwanza tangu 2015 licha ya kushuhudia ushindani mkali katika kitengo hicho kilichowajumuisha nyota wa Nigeria Burna Boy, Tyler ICU kutoka Afrika Kusini na raia wa Cameroon Labianca.
Tuzo hizo za kifahari za MTV Europe Music Awards, zilifanyika kwenye hafla ya kufana iliyoandaliwa Jumapili katika ukumbi wa Nord Villepinte, mjini Paris, Ufaransa.
Aidha, imekuwa ni usiku wa Platnumz kuweka historia kwani ubingwa huo umemfanya kuwa msanii wa kwanza wa Afrika kushinda tuzo za muziki za ulaya (EMAs) mara tatu kufuatia ushindi wake uliopita wa tuzo mbili za Best African Act & Best Worldwide Act (Africa/India) katika usiku mmoja kwenye MTV EMAs mnamo 2015.
Kufuatia ushindi huo, Diamond Patnumz amepokea pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa Na Michezo Gerson Msigwa.
Aidha, ubingwa huu wa Diamond Platnumz unadhihirisha ustadi wake kwenye mziki baada ya kushinda pia 2015 ambapo aliwapiku waimbaji wengine mashuhuri wakiwemo Yemi Alade, Davido, Dj Arafat, Indus Creed, Priyanka Chopra, na wengine kadhaa.