Kombe la Mataifa ya Afrika la mwaka 2023 limekuwa zaidi ya mashindano ya soka.
Mashabiki wanaokusanyika kwenye viwanja mbalimbali kutazama michezo wamegeuza tukio hili kuwa sherehe yenye rangi nyingi za kitamaduni, ikigubikwa na ishara tajiri za Kiafrika ambazo zinauza bara la Afrika kwa njia chanya katika jukwaa la kimataifa.
Katika mitandao ya kijamii, mashabiki kutoka ndani na nje ya bara wamekuwa wakistaajabia mavazi mbalimbali ya kuvutia.
''Mchezo huu umetukumbusha tena sisi ni akina nani. Sisi ni watu wenye furaha, sisi ni ndugu, sisi ni moja,'' aliandika shabiki mmoja @Pana kwenye X.
''Rangi nyingi sana'' alikubaliana @Awemih_Dave9 pia kwenye X.
Kama walivyosema, Kombe la Mataifa ya AFCON limekuwa sehemu ya mchanganyiko wa kitamaduni.
Kwa mchezo ulioletwa kutoka magharibi, mashabiki wamefanya juhudi kubwa kwa kila mchezo, wakijitahidi kuonyesha vipengele vya kitamaduni vya nchi zao.
''Sherehe zetu zote, rangi zetu, ngoma zetu, sio kwa ajili ya nchi yangu pekee, tunafanya hivi kwa ajili ya Afrika, kwa sababu Afrika ni kubwa,'' alisema shabiki mmoja wa soka wa Cape Verde kwenye Facebook.
Timu za taifa mbalimbali zinazoshiriki katika mashindano hayo pia zimeonyesha utajiri wa utofauti wa kitamaduni wa Kiafrika.
Mitandao ya kijamii ilijaa picha za timu mwanzoni mwa michezo ambapo wachezaji walitangaza kuingia kwao kwa mavazi ya Kiafrika yaliyobinafsishwa.
''Natumaini uhusiano huu, furaha hii, itadumu zaidi ya mchezo huu, kwa sababu Waafrika wanastahili kuwa na furaha,'' anasema shabiki mwingine, Anne, kwenye mitandao ya kijamii.