Meno yaliyopangika yanaweza kukupa ujasiri wa kucheka bila uwoga. / Photo: Getty Images

Je, umewahi kuwaza ni kitu gani kinaweza kukupa ujasiri wa kucheka mbele za watu? Mara nyingi afya ya kinywa hasa meno yaliyopangika vizuri na mdomo usiotoa harufu mbaya ndio vitu pekee vinavyoweza kukupa furaha, amani ya moyo na hata ujasiri wa kujiamini na kuangua kicheko mbele ya halaiki ya watu bila uwoga au wasiwasi wowote.

Wataalamu wa afya wanasema kwamba, afya ya kinywa licha ya kuboresha haiba na mtazamo wa mtu kwa nje, lakini pia ni muhimu kwa sababu inahusishwa na afya ya mwili mzima. Tena inashauriwa angalau mara moja kwa mwaka, kumuona daktari wa meno.

Magonjwa kama vile moyo, kisukari, upumuaji na hata changamoto nyengine za kiafya hunasibishwa na afya ya kinywa.

Licha ya umuhimu huo, lakini ni wachache wanaozingatia umuhimu wa utunzanji wa meno. Hii inaweza kuchangiwa na sababu kadhaa ikiwemo ukosefu wa elimu ya umuhimu wa kutunza meno, lakini baadhi ya nyakati pia, kushindwa kumudu gharama za matibabu ya meno ikiwemo kuweka meno bandia kutokana na gharama zake.

Meno Bandia ya Lab X | Picha: TRT Afrika

Tafiti zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu milioni 400 wanasumbuliwa na magonjwa ya meno barani Afrika, ambapo kuna mambo mbalimbali yanayochangia kuwepo kwa hali hiyo. Chanzo kikubwa kimeelezwa kuwa ni usafi duni wa meno, lakini pia matumizi ya kupitiliza ya vyakula vya sukari.

Kutokana na hali hiyo, vituo mbalimbali vinavyotoa huduma ya meno vimeanzishwa. Kwa mfano, katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, nchini Tanzania, kuna vituo zaidi ya 250 vinavyotoa huduma hizo. Hata hivyo, asilimia 90 ya vituo hivyo, vinaagiza meno bandia kutoka nchi kama vile China na hata India, hali inayofanya bidhaa hizo kuuzwa kwa gharama kubwa pindi zinapowasili nchini.

Bei Nafuu

Lakini je, ni wangapi wenye uwezo wa kumudu gharama za matibabu ya meno, ikiwemo kuweka meno bandia?

Meno Bandio ya Lab X na Alphonce | Picha: TRT Afrika

Dk Joshida Benjamin Cosmas ambae ni daktari wa meno jijini Dar es Salaam anasema bei ya meno bandia kutoka nje ya nchi ni kubwa hivyo wengi wanaotaka kuziba mapengo hushindwa kuhimili gharama.

"Kwa mfano, bei ya meno ya nje ni dola za kimarekani 350 hadi 900 huku kukiwa na adha ya kusubiri kwa zaidi ya mwezi mmoja hadi mitatu. Huku bei ya jino moja nchini Tanzania ni kuanzia elfu 30 hadi laki moja ambazo ni sawa na dola 20 mpaka 40," anaeleza Dk. Cosma.

Safari ndio imeanza kwa vijana hawa waliokuja na teknolojia ya ubunifu wa kisasa, lakini wanahitaji kuungwa mkono ili kukabiliana na baadhi ya changamoto. | Picha: TRT Afrika

Ni kutokana na changamoto hizo, ambapo baadhi ya vijana nchini Tanzania wameona ni vyema kuitumia fursa hiyo na kuleta ubunifu wa aina yake utakaosaidia jamii kwa ujumla.

Suluhu kwa njia ya teknolojia

Abbas Mshindo ambae ni mbunifu kutoka Lab X Technologies nchini Tanzania anasema kutokana na ubunifu wao wa kutengeza meno bandia, wameweza kutengeza meno bandia kwa haraka na bei nafuu.

"Tunaweza kutengeza meno bandia 18 kwa siku ambayo ni sawa na meno 126 kwa wiki," anasema Abbas na kuongeza kuwa, meno wanayotengeza ni rahisi kwa asilimia 80 ikilinganishwa na bei ya meno bandia yanayotoka nchi kama vile Dubai, India na hata China.

Safari ndio imeanza kwa vijana hawa waliokuja na teknolojia ya ubunifu wa kisasa, ambaao wanahitaji kuungwa mkono ili kukabiliana na changamoto zilizopo.

"Sekta ya afya ina vigezo vingi, ni jambo zuri, lakini tatizo ni mchakato wa bidhaa kuthibitishwa na mamlaka husika kuchukua muda mrefu," Abbas ameiambia TRT Afrika.

Lakini mbali na hivyo, Abbas pia anasema, uelewa bado ni mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia ya 3D katika kutengeza bidhaa hiyo.

"Hili limekuwa tatizo kwetu hata kupata wafanyakazi wenye uzoefu," anasema.

 kuna vituo zaidi ya 250 vinavyotoa huduma hizo. Asilimia 90 ya vituo hivyo, vinaagiza meno bandia kutoka nchi kama vile China na hata India 

Lakini siku zote wahenga wanasema, kinga ni bora kuliko tiba. Hivyo, njia bora inayopendekezwa na wataalamu ya kuzuia kuwepo au kukabiliana na tatizo la kinywa hasa meno, ni kuhakikisha usafi wa kinywa unafanywa kwa njia sahihi lakini vile vile kwa kutumia na dawa za meno zenye ubora.