Na Coletta Wanjohi
Tangu mwaka 2019, kila mwaka Melaku Hailu hupanga mfano wa mkutano wa marais wa Umoja wa Afrika huko jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Pamoja na vijana wengine ndani ya Ethiopia wanaoiga viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika wanajadiliana kama wakuu wa nchi wanavyofanya, na kutoa mapendekezo yao wenyewe, ambayo wanayawasilisha kwa Tume ya Umoja wa Afrika.
"Nilianza hivi ili vijana wengi zaidi waweze kufuatilia kwa karibu yale ambayo viongozi wetu wa Afrika wanajadili kila wanapokutana," Melaku Hailu, mwanzilishi wa Model AU-Ethiopia, anaiambia TRT Afrika, "kwa njia hiyo tutakuwa na vijana wengi wanaovutiwa na jinsi mambo yalivyo katika bara letu.
"Tunaamini kwamba ikiwa vijana wengi zaidi watafanya hivyo katika viwango tofauti katika nchi zetu za Afrika, tutaweza kuandaa kizazi baada ya kizazi kuhusika katika maendeleo ya bara letu," Hailu anasema.
Afrika ndilo bara changa zaidi duniani lenye watu zaidi ya milioni 400 wenye umri kati ya miaka 15 na 35. Umoja wa Afrika unaojumuisha nchi 55 za Afrika baada ya muda umetambua uwezo wa vijana.
Viongozi wa Afrika walitenga mwaka wa 2017 kwa ajili ya uwekezaji kwa vijana.
"Wakati Afrika iilikuwa inaunda Jumuiya za Umoja wa Afrika miongo kadhaa iliyopita vijana walikuwa wakionekana kuwa watu wa kufanya tu machafuko, lakini siku hizi viongozi wa nchi wanawajumuisha katika michakato muhimu ya maamuzi katika ngazi tofauti, kwa sababu Afrika haiwezi kuendelea bila vijana," Neema Chusi, Mkuu wa Ofisi ya Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika, anaiambia TRT Afrika.
Mnamo 2022, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa yaani Africa CDC, iilitumia vijana chini ya mpango unaoitwa "Bingwa Initiative" kuhamasisha jamii kupata chanjo ya Uviko-19 Umoja wa Afrika umeelezea wazo hilo kama "mafanikio".
Kuwawekea vijana jukwaa
Umoja wa Afrika unapofikisha miaka 60 mkazo wake ni zaidi katika kukuza hali ya kujitegemea na kujielekeza kwenye biashara zaidi kati yao, na vijana ndio kitovu cha dira hii.
"Kuna imani thabiti kwamba maendeleo ya bara hili yanaweza kupatikana kwa kweli tu kwa kubadilisha faida linganishi ambayo ni ongezeko la vijana kuwa mgawanyiko wa kidemografia," anasema Wamkele Mene Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.
Huu ni mpango Mkuu wa Umoja wa Afrika unaolenga kukuza zaidi biashara ya ndani ya Afrika.
"Ni muhimu kuwawezesha vijana katika nyanja zote za maisha kwani kuwaacha vijana bila vifaa na bila fursa kutahatarisha maendeleo jumuishi na endelevu ya bara," Wamkele anasema.
Carlos Lopes, Katibu Mtendaji wa zamani wa tume ya Umoja wa Mataifa yaani UN ECA anasema Afrika yenye idadi kubwa ya vijana iko katika nafasi nzuri ya kustahimili mielekeo mikubwa mitatu ambayo itaathiri siku zijazo: idadi ya watu, mabadiliko ya hali ya hewa na teknolojia.
"Kwa kawaida watu wanadhani uvumbuzi unafanyika mahali pengine, wa kidijitali na wa aina tofauti lakini habari ni kwamba, michakato ya kiufundi na bidhaa zinazidi kuwa za kuvutia zaidi kwa vijana hapa barani” anaiambia TRT Afrika.
"Hii inamaanisha kuwa soko la watumiaji wa Afrika litakuwa la kuvutia zaidi katika takriban muongo mmoja hivi na ndiyo maana unaona maboresho yote ya kusaidia wanayoanza ili kuwa na utayari kuzalisha ndani ya Afrika," Lopes anaongeza.
Vijana barani Afrika wanajua wanachotaka
Mjumbe wa Vijana wa Umoja wa Afrika ameutaka Umoja wa Afrika kupitia upya mkataba wa vijana wa "ili kufikia hali halisi ya sasa inayowakabili vijana barani Afrika".
Mkataba huu wa vijana uliopitishwa mwaka 2006 na marais wa Afrika unalenga kutoa mwanya wa ushiriki mzuri wa vijana katika mchakato wa maendeleo.
"Viongozi wetu wa Kiafrika kama Kwame Nkrumah na wengine, walipokuwa wakipigania uhuru wa bara letu, hawakuwa na aina ya teknolojia, mawasiliano na udhihirisho kama sisi sasa," Hailu mwanzilishi wa Model AU-Ethiopia anaiambia TRT Afrika.
"Hivyo haijalishi vijana wako wapi barani, wanaweza kutumia aina yoyote ya teknolojia na kupaza sauti kuhusu mawazo yao na hata kuweza kujiajiri,” Hailu anasema.
Badru Juma Rajabu, kijana kutoka Tanzania anasema kuna manufaa ya nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika vijana. Badru ni kiongozi wa vijana katika shirika la Restless Development, nchini Tanzania.
Restless Development ni shirika la kimataifa linalowahimiza vijana kutumia uwezo wao wa ujana na kufanya mabadiliko katika jamii.
"Kijana mmoja anapopata kazi, tuna uhakika kwamba angeweza kusaidia familia mbili au tatu, hasa kwa sisi ambao tunatoka katika familia kubwa," Rajabu ameiambia TRT Afrika.
"Elimu ya sasa tunayozungumzia inapaswa kuboreshwa na ili kuwasaidia vijana kusaidia jamii zao zaidi," amesema, "pia tunahitaji huduma za afya za bei nafuu. Leo hii huwezi kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa na kutozungumza kuhusu vijana."
"Kwa sababu ikiwa asilimia 75 ya idadi ya watu barani Afrika ni ya vijana lazima wawepo vijana mezani ili kuchangia mijadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi na wachukuliwe kama viongozi . Hii itasaidia kuwafanya kutumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi,” Rajabu ameongezea TRT Afrika.
Wataalamu wanasema bara la Afrika linahitaji kuwa na maksudi katika kutekeleza sera zitakazosaidia vijana kutoka ngazi ya chini kutumia rasilimali zilizopo kujiimarisha.
Afrika ina dira ya maendeleo, inayoitwa Agenda 2063 inayotaka kuweka bara katika njia ya kimaendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Vijana wa Afrika wanasema miaka 40 haiko mbali na bara linahitaji kuwekeza zaidi kwa vijana wake ili kufikia Afrika inalotaka.