Safari ya kutia moyo ya Melisa Metin, mshichana mwenye umri wa miaka 18, ambaye amegeuka kutoka kuwa mhudumu wa usafi wa Chuo Kikuu cha Inönü Turgut Özal nchini Uturuki, hadi kuwa mwanafunzi wa udaktari, imewaacha wengi vinywa wazi nchini Uturuki.
Metin alisema kuwa atafanya kazi hospitalini zamu ya usiku na pia atafanya kazi hiyo huku akiendelea na masomo yake.
"Walimu wetu wanasema 'wewe ni mwanafunzi wetu na mfanyakazi wetu'. Ninafurahi sana. Wananipenda. kwa kweli, ni jambo zuri, napenda kufanya kazi ya kusafisha. Natumani kufanya kazi pia kama daktari," anasema Melisa.
Melisa amejiunga na wanafunzi wenzake wiki hii na kuanza masomo ya udaktari katika Chuo Kikuu hicho baada ya kufanikiwa katika Mtihani wa Taasisi ya Elimu ya Juu (YKS) na kushinda nafasi kwenye kitengo cha udaktari katika chuo kikuu chicho hicho.
"Baada ya mtihani wa kusaka nafasi katika Chuo Kikuu, nilikuja hospitali na kufanya usajili wangu wa kuomba kazi. Niliwasilisha nyaraka zangu kwa ajili ya kazi. Baada ya kupokea ujumbe na matokeo yangu kwa njia ile ile, nilianza kufanya kazi mnamo Agosti," anasema.
Melisa Metin alisema kuwa alifanya mtihani wa KPSS alipokuwa akishiriki mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili na akapata alama 80 katika mtihani huo, na baadaye akaomba kuajiriwa kuwa mfanyakazi wa Chuo cha Matibabu cha Turgut Ozal kabla ya tetemeko la ardhi la tarehe 6 mwezi Februari mwaka huu.
Tetemeko hilo la ardhi lilisababisha uharibifu mkubwa darasani na kuathiri maandalizi ya Melisa huku akilazimika kuenda kujiandaa kwa mitihani ya chuo kikuu, nyumbani.