Na Charles Mgbolu
Akiwa amevalia gauni jekundu na kofia na tabasamu pana, mwigizaji mkongwe wa Afrika Kusini mwenye tuzo nyingi Sello Maake Ka-Ncube alipiga picha baada ya kupokea tuzo yake ya heshima ya udaktari mwishoni mwa juma.
Tuzo hiyo ilitolewa na Chuo Kikuu cha Trinity International Bible mnamo Jumamosi, Aprili 20. Muigizaji wa The Man in the Mirror alichapisha picha kadhaa za sherehe hiyo kwenye mtandao wa "X" na kujitambulisha kwa fahari kuwa ni Daktari Sello Maake kaNcube.
Lakini hafla hiyo ya utoaji tuzo imeitwa ya "udanganyifu" na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Blade Nzimande.
Nzimande, kupitia kwa msemaji wake, Veli Mbele, alisema Chuo Kikuu cha Trinity International Bible hakina kibali cha kutoa tuzo yoyoote kwa sababu si taasisi ya elimu ya juu iliyosajiliwa binafsi.
“Tuliwahi kuandikia Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Trinity hapo awali na kuwaonya kuhusu kuendelea kufanya kazi kinyume cha sheria na kuhalalisha shughuli zao. Pia tumeliomba Baraza la Elimu ya Juu (CHE) mwongozo kuhusu jinsi sifa za heshima zinapaswa kutolewa na nani,’’ Nzimande alisema katika taarifa yake Jumatatu.
‘’Idara inazingatia hatua za kina zaidi na madhubuti dhidi ya Chuo Kikuu cha Trinity International Bible na watu wengine wote au taasisi zinazoendelea kuhujumu kanuni za idara,” Nzimande aliongeza.
Hatua hiyo iliibua mijadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakionesha dhihaka kutokana na tukio hilo.
‘’Nina shauku ya kujua kwa vile sioni jina la chuo kikuu na kuona sherehe jinsi ilivyokuwa ,’’ aliandika shabiki, @IKEKHUMALO2, kwenye ukurasa wake wa X.
“Ni lini vyuo vikuu vitaanza kufungia vyuo vikuu venye kutoa shahada tata?” aliuliza shabiki mwingine Nicola, kwenye X.
Sello sio mtu maarufu pekee nchini Afrika Kusini kutunukiwa shahada ya heshima na chuo hicho chenye utata siku ya Jumamosi.
Mwigizaji wa Afrika Kusini Elizabeth Serunye aliweka picha mtandaoni ikumuonesha amevalia joho kofia ya mahafali na kuandika kwenye Instagram yake, ‘’Ni siku ya mahafali. Sasa ni rasmi, Dk Sikasu Serunye.’’
Mwimbaji wa nyimbo za Injili Winnie Mashaba pia alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari kutoka taasisi hiyo mwaka 2019.
Si Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Trinity wala Sello Maake Ka-Ncube ambao wametoa maoni yoyote kufuatia maendeleo haya.
Picha za Sello, Elizabeth, na Winnie zilizopigwa kwenye sherehe hizi zenye utata za tuzo pia hazijaondolewa kwenye mitandao ya kijamii.