Kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa yaani Afrika CDC, inasema visa vya kipindupindu nchini Malawi vinapungua. Kipindupindu husababishwa na unywaji wa chakula au maji ambayo yamechafuliwa na bakteria inayoitwa ‘Vibrio cholerae’.
Katika kipindi cha wiki ya tarehe 16 mpaka 23 mwezi Machi, Malawi imeripoti visa vipya 1,345 pamoja na vifo 34, tofauti na wiki iliyopita ambapo viliripotiwa visa 3,694 pamoja na vifo vipya 76 kutokana na kipindupindu, Africa CDC imefafanua.
"Visa vya kipindupindu vinapungua kwasababu ya juhudi za pamoja za serikali na mashirika ya nje kama Africa CDC," anasema dkt. Ahmed Ogwell, kaimu Mkurugenzi wa Afrika CDC. "Nguzo mbili muhimu za kupunguza kipindupindu ni kuhakikisha kuwa chanzo chako cha maji ni safi na pili utupaji wa uchafu ni kwa njia ambayo haichanganyiki na maji."
Je, tunajua nini kuhusu Kipindupindu Kusini mwa Afrika?
Malawi ni mojawapo ya nchi 14 barani Afrika zilizoathiriwa na kipindupindu.
•Nchi zilizoathirika ni pamoja na Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe
•Malawi ina asilimia 66 ya visa vyote vya kipindupindu barani Afrika huku zaidi ya visa 50,000 vilivyothibitishwa tangu kuzuka kwa ugonjwa huo mnamo Februari 2022.
• Kimbunga cha kitropiki Freddy kilichoanza Februari 2023 kimesababisha mafuriko nchini Malawi na Msumbiji na kuharibu baadhi ya vituo vya usafi
• Zambia yenye kesi zaidi ya 225 hadi sasa iko hatarini kwa sababu ya soko liilopo katika mpaka na Malawi