Mpacha walioungana Hassan na Hussein ambao wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali maarufu ya watoto ya Mfalme Abdullah, wamefanyiwa uchunguzi muhimu na wataalam mbalimbali wa watoto huku wakitoa taarifa chanya ya uwezekano wa kuwatenganisha kwa upasuaji kwa mafanikio.
Watoto hao kutoka Tabora, waliwasili Saudi Arabia Agosti 24 Agosti, mwaka huu, na walifanyiwa ukaguzi na wataalamu kama vile madaktari wa upasuaji wa kupandikiza yaani plastick surgery ya watoto, daktari bingwa wa Ubongo na mabingwa wa neva.
Daktari maarufu Zaituni Bokhari, Daktari wa upasuaji wa watoto katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Tanzania, amekuwa akishirikiana kwa karibu na madaktari wa Saudia katika taratibu zote za kuwatenganisha Hassan na Hussein.
Daktari Zaituni amekuwa akiwashughulikia mapacha hao na kuwaangalia kwa karibu tangu alipowapokea na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa takriban miaka miwili baada ya kuletwa kutoka magharibi mwa Tanzania wiki mbili tu baada ya kuzaliwa hadi waliposafirishwa kwenda Riyadh.
Upasuaji wa watoto hao ulihitaji utaalamu wa hali ya juu katika maeneo mbalimbali kwani kulingana na madaktari, mapacha hao Hassan na Hussein wameungana kifuani, tumboni, nyonga, utumbo mpana na puru, huku upasuaji wao ukionekana kuhitaji ustadi mwingi.