Viongozi wa mataifa jirani wa Sudan wamewasili mjini Cairo, Misri, kushiriki mkutano wa marais wa kutafuta suluhisho la mzozo unaoendelea nchini humo.
Hatua hiyo, ikiwemo mojawapo ya juhudi mbalimbali za kusimamisha mapigano nchini Sudan yanayoendelea kwa mwezi wa tatu sasa, inajiri huku Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, likisema kuwa vita hivyo vimewaacha zaidi ya watu milioni 3 bila makao, wakiwemo watu 700,000 waliokimbilia nchi jirani.
Miongoni mwa viongozi hao ni marais Idriss Déby wa Chad, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Isaias Afwerki wa Eritrea, na Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia, mataifa jirani yaliyopokea idadi kubwa ya wakimbizi wa Sudan.
Rais wa Misri Abdel-Fattah El-Sisi ndiye mwenyeji wa mkutano huo, huku nchi yake ikiwa taifa lililowalaki wakimbizi wengi zaidi wa Sudan kwani asilimia 60 wa raia wa nchi hiyo waliokimbia machafuko wamepokewa nchini Misri.
Kulingana na Shirika la IOM, asilimia kubwa ya watu waliokimbilia nchi jirani ni raia wa Sudan huku wengine wakiwa ni raia wa nchi zingine huku wengi wakilazimika kukimbia makwao.