Juhudi mingi za kusitisha vita nchini Sudan hazijafaulu  / Photo: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Wakimbizi, mgogoro wa kibinadamu, na vita ni masuala ambayo sasa yanaizunguka Sudan.

Nchi ambayo ilikuwa katika njia ya kurejea katika utawala wa kiraia huku uchaguzi ukipangwa kufanyika 2024, baada ya kuondolewa madarakani kwa Omal El Bashir mwaka wa 2019.

Matumaini hayo yanapungua huku mapigano mapya ya kijeshi kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid support Forces yaliyoanza tarehe 15 Aprili 2023 yakiendelea.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni 1.4 hawana pa kurejea nyumbani.

"Ni asilimia 20 tu ya vituo vya afya huko Khartoum ambavyo bado vinafanya kazi, hali ambayo inaonyesha kuanguka kwa mfumo wakati unapohitajika zaidi," alisema Alfonso Verdu Perez, mkuu wa ujumbe wa ICRC nchini Sudan.

Wale ambao wamefanikiwa kuikimbia nchi hiyo wametafuta hifadhi kati nchi jirani za Sudan Kusini, Chad, Misri au Ethiopia.

Wizara ya Afya ya Shirikisho la Sudan imesema takriban watu 730 wameuawa, na takriban 5,500 wamejeruhiwa kote nchini tangu tarehe 15 Aprili.

Na hali inaelekea kuwa mbaya zaidi kwa sababu Jenerali Abdel Fattah al-Burhan wa Jeshi la Sudan na jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, mkuu wa vikosi vya Rapid support Forces hawajaamua kunyamazisha silaha zao,

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anaongea na wanajeshi jijini Khartoum.

Wito wa kusitisha mapigano

Kumekuwa na angalau juhudi 10 za kusitisha mapigano kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid support Forces haswa ili kuruhusu usambazaji wa mahitaji ya kibinadamu kuwafikia watu walioathirika,

Jaribio la kwanza la kusitisha mapigano lilikuwa tarehe 16 Aprili, siku moja baada ya mapigano kuanza, wakati mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Sudan, Volker Perthes alitoa wito kwa pande zote kuwacha vita angalau kwa masaa machache.

Pande zote mbili hazijaheshimu makubaliano au wito wa usitishaji vita kikamilifu.

"Ikiwa bado majenerali hao wawili wanaendelea kupata faida wanaona ni bure kuacha kupigana," Tibor Nagy, Katibu msaidizi wa zamani wa Marekani katika Afrika anaiambia TRT Afrika.

"Jeshi la Sudan lina jeshi la anga na wana vifaru vizito vya vita lakini kikundi cha RSF kimekita kambi maeneo ya watu , wako katika eneo la mijini ,na wana kituo chao huko Darfur kwa hivyo jumuiya ya kimataifa haiwezi kufanya kitu hadi viongozi hao wawili wawe tayari, ” anaeleza Nagy.

Majenerali hao wanaopigana hawakuheshimu hata wito wa kusitishwa kwa mapigano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuheshimu mwezi mtukufu wa Ramadhan mwezi Aprili.

"Ili usitishaji wa mapigano uendelee, usitishaji huo wa mapigano unahitaji wadhamini kuwawajibisha watu ambao wametia saini mkataba huo," anasema Dkt.Edward Githua, mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa.

Tarehe 20 Mei mwaka huu Saudi Arabia na Marekani ziliwezesha kusimamia pande hizo mbili zikatia saini makubaliano ya usitishaji vita wa muda mfupi huko Jeddah, Saudi Arabia.

Usitishaji huu wa mapigano, tofauti na wengine, ulikuwa na utaratibu wa ufuatiliaji lakini bado mapigano yaliripotiwa ndani ya siku saba zilizokubaliwa.

Mnamo tarehe 30 Mei pande hizo mbili chini ya uwezeshaji wa Marekani na Saudi Arabia ziliwezesha kurefushwa usitishaji mapigano kwa siku nyingine tano.

Lakini siku moja tu baadaye jeshi la Sudan lilisitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya kusitisha mapigano likiwashutumu watu wa upande huo mwingine kwa kushindwa kutimiza ahadi zao.

Je, vikwazo vinaweza kuwa na athari?

Marekani ilijitokeza kama mwezeshaji wa makubaliano ya wanaopigana Sudan huku jumuiya ya kimataifa ikitafuta suluhu ya kudumu la mzozo nchini Sudan.

Pamoja na Saudi Arabia imewezesha makubaliano kadhaa kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi Rapid support Forces.

Tarehe 4 Mei 2023 rais wa Marekani Joe Biden alitia saini amri ya utendaji ya kuweka ya kuwawekea vikwazo watu wanaohusika na ghasia nchini Sudan.

"Vikwazo ni njia mojawapo ambayo inaweza kuwalazimisha watu hawa angalau kupunguza mapigano kwa sababu ikiwa hautapata "hatua yao dhaifu " au mahali ambapo wako hatarini na ukiwashikilia kwa mazingira magumu wataendelea kupigana,"Githua anaiambia TRT Afrika.

Lakini hata tishio la vikwazo haujalazimisha kukomesha mapigano.

"Tatizo ni kwamba unaweza kuweka vikwazo vingi lakini ni kiasi gani itawaumiza ikiwa wana njia kando na mfumo wa dola ili kuuza dhahabu yao?" anauliza Nagy.

Usitishaji wa vita nchini Sudan kutawawezesha wananchi kupata mahitaji muhimu ya maisha

Umoja wa Afrika unasisitiza kuwa mchakato wa amani nchini Sudan lazima uwe mchakato unaoongozwa na Sudan, na pia umeonya aina zote za uingiliaji wa nje nchini Sudan.

"Kwa kweli kuna uingiliaji kutoka nje ya Sudan kwa sababu Sudan inapakana na nchi 7 na upande wa kulia ni bahari Nyekundu hivyo kila nchi moja inataka rasmi mapigano yasitishwe lakini kwa njia isiyo rasmi wana upande amabao wanapendelea," anasema Nagy.

"Pia kuna changamoto kwa nchi ambazo zinamuunga mkono jenerali mmoja au mwingine, kama tunaweza kupata wasaidizi hawa wa nje pia kujishusha na kuacha kuwaunga mkono majenerali kunaweza kuwa na nafasi ya kusitishwa kwa mapigano haya,” Githua anaiambia TRT Afrika.

AU inasema mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, "atatuma wajumbe kwa mataifa jirani ya Sudan kama sehemu ya juhudi zake za kuimarisha utafutaji wa mbinu ya pamoja ya kutafuta suluhu endelevu kwa mgogoro wa tabaka nyingi nchini Sudan."

Juhudi za pamoja za kutafuta suluhu zinaendelea kati ya Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali, IGAD.

"Kuwepo kwa mipango mbali mbali ya upatanishi haitatumikia maslahi ya matakwa ya pamoja ya watu wa Sudan," anasema Dkt. Workeneh Gebeyehu, katibu mtendaji wa IGAD.

Lakini juhudi zao zinakabiliwa na changamoto

Jeshi la Sudan katika barua iliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa limeomba kujiuzulu kwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu (SRSG) Volker Perthes anayeongoza Misheni ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi wa Mpito nchini Sudan (UNITAMS).

Hadi Jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid Support Forces watakapokubali kuweka silaha zao chini kabisa , raia wa Sudan wanaendelea kujiuliza ni lini watapata amani na maisha ya kawaida chini ya utawala wa kiraia.