Watoa Huduma za Usalama Binafsi watahitaji mafunzo katika masuala ya usalama kama hitaji la lazima la usajili na leseni. Picha: Wizara ya Usalama wa ndani.

Shughuli za usajili wa walinzi wote binafsi nchini Kenya imeanza rasmi leo huku Serikali ya nchi hiyo kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Usalama Binafsi, ikitaja hatua hiyo kuwa ni katika jitihada za kuimarisha uwajibikaji na kuleta mabadiliko kwenye utendaji wa sekta hiyo.

Walinzi hao binafsi wapatao zaidi ya 500,000 pamoja na waajiriwa wao sasa watalazimika kutekeleza uamuzi huu mpya baada ya Wizara ya Ulinzi wa ndani kufanya uzinduzi wa zoezi la usajili, mjini Kisumu, kupitia Katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama wa ndani Dkt Raymond Omollo na Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usalama Binafsi, Fazul Mahamed.

Miongoni mwa watakaosajiliwa chini ya hatua hii na kupewa leseni ni pamoja na Wataalamu wa Usalama Binafsi, Maafisa Usalama wa makampuni, washauri wa Usalama, wachunguzi binafsi, walinzi Binafsi na maofisa wa usalama binafsi walioajiriwa na Taasisi za Serikali, makampuni ya ulinzi, vyombo vya ushirika na watu binafsi.

Pindi mlinzi atakapokamilisha usajili, atapokea nambari ya usalama, nambari ya kipekee ya utambulisho kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Usalama binafsi PSRA kama uthibitisho wa kuwa amepokea mafunzo, kusajiliwa na kupewa leseni kama mtoa huduma binafsi wa usalama.

TRT Afrika