Coletta Wanjohi
Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali, IGAD, imesisitiza upya wito wake wa msaada zaidi wa kibinadamu kwa kanda hiyo huku ukame na uhaba wa chakula ukiendelea .
Shirika hilo la kikanda limesema katika taarifa kwamba watu milioni 47 wameathiriwa na mvua ya chini ya wastani tangu mwaka 2020.
Inasema katika sehemu za Ethiopia, Kenya, na Somalia "hatari ya njaa ni ya kweli na sio masihara".
"Kurejea kwetu kwa hali ya kawaida kutahitaji rasilimali na muda," Mkurugenzi Mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu amesema.
Kulingana na kituo cha utabiri wa hali ya hewa cha IGAD, yaani ICPAC, watu milioni moja wameyakimbia makazi yao na kanda imesajili zaidi ya vifo milioni 10 vya mifugo na wanyamapori.
ICPAC ni Kituo cha hali ya hewa cha kikanda ambacho hutoa huduma za hali ya hewa kwa nchi 11 za Afrika.
IGAD inasema dola za Marekani milioni 710 zinahitajika katika miezi minne ijayo kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu Ethiopia, huku Kenya ikihitaji dola za Marekani milioni 378 ili kutoa chakula, maji na chanjo kwa kaunti zilizoathirika hadi Oktoba 2023.
Somalia kwa upande mwingine inahitaji dola za kimarekani bilioni 1.6. ili kutoa msaada wa kibinadamu kwa walioathirika.