Ukisafiri barabara za kaunti ya Migori, Magharibi mwa Kenya, bila shaka utaona mandhari ya kuvuti aya mashamba makubwa yaliyojaa mimea, na matunda ya kupendeza na mboga. Ni eneo lililo na rotuba sana.
Lakini, akiwa shambani mwake, Robert Opar, mwenye umri wa miaka 40 ana huzuni kubwa kukumbuka utotoni mwake akimsaidia baba yake shambani. Kwa miaka mingi walikuza tumbaku katika shamba lao la ekari tatu. Lakini kilimo hicho kilimtibulia nyongo baba yake.
‘‘Nilimpeleka baba yangu hospitalini, alipolalamika kuwa na maumivu ya kifua. baada ya kiumfanyia uchunguzi, daktari aliniuliza iwapo baba alikuwa mvutaji wa sigara. Nilimwambia la, ila alikuwa akitafuna majani ya tumbaku. Daktari aliniambia hilo lilimsababishia matatizo ya figo.’’
Bwana Opar ameambia TRT Afrika kuwa hiyo ndio siku alichukia kilimo cha tumbaku.
‘‘Niliona kuwa hii haina uzuri wowote kwangu. Lazima niachane nayo,'' alisema.
Baba yake alifariki miaka michache baadaye.
Hatari za kilimo cha tumbaku
Tumbaku kwa jumla imeonesha madhara zaidi ya manufaa. Uvutaji wa sigara, inayotokana na tumbaku, unaweza kukusababishia maradhi ya mfumo wa kupumua pamoja na saratani ya mdomo au mapafu.
Lakini kwa mujibu wa WHO, kilimo cha tumbaku kinaweza kuwa na madhara kwa afya ya wakulima ambao wanalazimika kugusa majani yake au kupumua hewa ya sumu kutoka kwa mmea huo.
Zao hilo pia linaaminiwa kuwa haribifu kwa radhi kwani inakunywa viritubishi kupita kiasi na kuacha shamba likiwa tasa.
‘‘Unapolima tumbaku, inakuachia ardhi tasa.'' anasema Opar.
Huwezi kuza kitu kingine tena hapo kwa muda wa miezi sita, lazima uiache ardhi ipumue. Kwa hiyo unaingia hasara tu,'' anaongeza.
Geukia kilimo chenye afya
Bwana Opar anasema kuwa sasa ameachana na kilimo cha tumbaku kwa ajili ya afya ya familia yake, na pia pato lake limekuwa la kuridhisha.
‘‘Sasa nalima pilipili mboga, tikiti maji na maharage. Nilifanya utafiti mwanzo lakini nimeridhika na uamuzi wangu.'' anasema. '' Wakati mwingine watu wanaagiza bidhaa zangu shambani kabla hata ya kuvuna, napata pesa ya kutosha sasa.''
Kenya ni miongoni mwa nchi za kwanza saini mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya udhibiti wa zao la tumbaku na kisha ikapitisha sheria iyo nchini. Nyaraka hizo mbili zinasisitiza umuhimu wa kuwa na zao mbadala ili kuhifadhi rasilimali ya wakulima wanaotegemea kilimo chake.
Mr Opar, pamoja na baadhi ya jirani zake wamejiunga na mradi wa kwa jina Tobacco Free, unaolenga kuwasaidia wakulima kupanda maharage yenye madini ya chuma ya hali ya juu kama zao mbadala, huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakitoa mwelekezo, mafunzo na kuchangia mbegu na mbolea, pamoja na ushauri wa mauzo.
Kaunti ya Migori nchini Kenya ni miongoni mwa kaunti tatu zinazozalisha tumbaku kwa kiwango cha juu zaidi. Zao hilo la kibiashara linachangia chini ya asili mia moja ya pato la taifa, na kuwaacha wakulima wengi katika umaskini.
Nchi zipi zinakuza tumbaku Afrika
Uzalishaji wa majani ya tumbaku duniani imepungua kwa kiasi kikubwa kati ya 2012 na 2018. Hata hivyo mauzo ya zao hilo kutoka Afrika yamekithiri kwa zaidi ya 10%, huku Afrika Mashariki ikizalisha zaidi ya 90% ya tumbaku ya Afrika.
Nchi za Afrika zinazokuza tumbaku kwa kiasi kikubwa zaidi ni Zimbabwe (25.9%), Zambia (16.4%), Tanzania (14.4%), Malawi (13.3%) na Msumbiji (12.9%).
Mwaka huu shirika la afya duniani, WHO, imetoa kaulimbiu ya 'Tunahitaji chakula, sio tumbaku,' kwa lengo la kuhamasisha juu ya kilimo mbadala na mauzo ya mazao ya wakulima hao ili kuwapa motisha kukuza vyakula vilivyo na virutubishi vya manufaa.
Bwana Opar anasema kuwa ana tamani angeachana na tumbaku mapema zaidi.
‘‘Tulikuwa na msitu mkubwa shambani kwetu. Miti mingi ilikatwa kwa ajili ya kukausha majani ya tumbaku. Sasa huwezi kuamini kulikuwa na msitu hapa.’’
WHO inasema kuwa athari zinazotokana na kilimo cha tumbaku zinajitokeza zaidi katika mataifa yanayostawi na yale maskini duniani.
Siku ya kupinga tumbaku duniani 2023 itatumika kama fursa kwa serikali na washika dau kuwasaidia wakulima katika kuwekamazingira muafaka ya kilimo cha afya ili kuhakikisha usalama wa chakula duniani.