Na Charles Mgbolu
Akiwa amesimama mbele ya ukumbi uliojaa watu katika eneo la Jukwaa huko Birmingham, UK, nyota wa muziki kutoka Nigeria Adekunle Gold alisimamisha bendi yake kwa muda ili kuongelea swala lenye ujumbe wa kutia moyo.
Mwanamuziki huyo mwenye miaka 37, anayejulikana kwa wimbo wake ‘’Party no dey stop’’, ambaye kwa sasa yuko katika ziara ya Ulaya kuitangaza albamu yake, alisema anataka kuwa mwangaza wa matumaini kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa seli mundu.
‘’Kwa wanajamii wa selimundu, mashujaa kwa yale wanayopitia. Nataka kusema unaweza kufanya hivyo. Kama ninawezyeweza, na wewe unaweza,’’ alisema huku akishangiliwa kwa vigelegele na hadhira yake tarehe 24 Februari.
Ilikuwa mwezi Julai 2022 ambapo Adekunle alishiriki kwa mara ya kwanza mapambano yake kama mtu anayeishi na selimundu.
Hii ni hali ya kurithi ya damu inayosababisha viwango vya chini vya oksijeni kwenye damu na kubana kwa mishipa ya damu, ambavyo vinaweza kusababisha maumivu makali mwilini pamoja na maambukizi makali ya bakteria, kulingana na WHO.
Takriban watoto 1000 wanazaliwa na ugonjwa huo kila siku barani Afrika, na kuufanya kuwa ugonjwa unaorithiwa kijenetiki ulioenea zaidi katika eneo hilo.
Zaidi ya nusu ya watoto wenye ugonjwa huo hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano, wanasema WHO.
Katika jarida moja akiongea na mashabiki wake mwezi Julai 2022, Adekunle alielezea kwa kina usiku wa maumivu na jinsi wakati mwingine alijitakia kifo.
"Moja ya migogoro mikali niliyowahi kuwa nayo ilikuwa nikiwa na umri wa miaka 20. Nakumbuka nikiwa nimelala kitandani katikati ya usiku, nikiomba yote yaishe. Nilimuomba Mungu achukue maisha yangu," aliandika.
"nahisi kama ukombozi hatimaye kuweza kushiriki sehemu hii ya maisha yangu na nyinyi, hatimaye kuweza kusema ukweli wangu. Ninapozungumzia jinsi nilivyopambana kufika nilipo leo, ninataka mjue kwamba mapambano yangu yalikuwa ya kweli."
Msukumo wa wimbo
Kuishi na ugonjwa wa seli mundu ni msukumo nyuma ya wimbo wake maarufu 'Five star' ambapo anawahimiza mashabiki wake kufikia ubora wao na wala wasiruhusu mazingira yaamue hatima yao.
Adekunle Gold, aliyeshinda Tuzo ya Msanii Mpya Bora katika Tuzo ya Burudani ya Nigeria mwaka 2015, si pekee anayesambaza ujumbe wenye nguvu kama huu kwani burudani zaidi zinaanza kufunguka kuhusu kukabiliana na changamoto ngumu za maisha ambazo mashabiki wanazipongeza kama za kumotisha.
Wasanii wawili wa Nigeria, Augustine Miles Kelechi (Tekno), Olamide Adedeji, na nyota wa muziki wa Tanzania Diamond Platnumz, ni mifano; wote wameongelea wazi nyakati ngumu walipopambana na afya yao ya akili.
Kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wamemsifu Adekunle kwa uwazi wake na jinsi anavyoendelea kuwa chanzo kikuu cha msukumo.
‘’Mungu akubariki, Adekunle Gold. Tufanye la maana mahali tulipo. Ikiwa unafikiri kile maisha yalivyokupa ndio mbaya zaidi, unakosea. Kila mtu alikuja hapa na mzigo wake,'' aliandika @retireesnigeria kwenye YouTube.
Shabiki mwingine, @omololaesho1210 pia aliandika kwenye YouTube: ‘’Hadithi ya ajabu sana.... Natamani mwanangu angeona na Adekunle angeongea naye na kumtia moyo....upendo mwingi’’
Somo Kwa wengine
Mashabiki wengine waliwahimiza watu mashuhuri wawe makini zaidi katika kuwasaidia mashabiki kuelewa kwamba kuna zaidi maisha nyuma ya fahari na anasa na kukubali ni sawa kuwa dhaifu.
‘’Tunapata msukumo kutoka hadithi kama hii. Inasaidia kujua kwamba hatuko peke yetu tunapokabiliana na changamoto za maisha, hivi ndivyo watu mashuhuri wanapaswa kuwa… mabalozi wa matumaini’’ aliandika @realakan pia kwenye Youtube.
Adekunle anasema ataendelea kusaidia watu, hasa wale wanaoishi na ugonjwa wa seli mundu, kuvuta nguvu kutoka hadithi yake mwenyewe na kamwe wasikate tamaa.
‘’Kwa hivyo hii ni kuwashabikia kila mtu anayepitia au kulazimika kukabiliana na maumivu yote na pambano la [seli mundu]. Unaweza kufanya hivyo. Haipaswi kamwe kukuzuia. Angalia mimi; mimi ni nyota mkubwa sasa hivi,’’ alisema katika tamasha lake la London.
Ziara ya Adekunle Gold nchini Uingereza inaendelea na onyesho lijalo huko Wembley tarehe 3 Machi huku msanii huyo wa Afrobeats akiendelea kuhamasisha wengi.