Luckmore na dadake Peace wamesifiwa kwa ujasiri wao. Picha Emmerson Mnangagwa

Na

Charles Mgbolu

Jumapili, tarehe 3 Machi, 2024, Luckmore Magaya mwenye umri wa miaka 12 na dada yake mdogo Peace mwenye umri wa miaka 10, walikaribishwa katika chumba cha mkutano cha Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, ambaye aliwakumbatia watoto hao kwa furaha.

Luckmore na Peace walikuwa wanatunukiwa kwa kitendo chao cha kishujaa, ambapo walikabiliana na mamba mkubwa ambaye alikuwa amemkamata mama yao kwa meno yake na kumvuta hadi mtoni.

Rais alisema alikuwa anawazawadia watoto hao $5000 kila mmoja kwa kukabiliana na kifo na kuokoa maisha ya mama yao.

Tukio hilo lilitokea miezi miwili iliyopita kando ya Mto Mupfure huko Mhondoro, kilometa 114 magharibi mwa mji mkuu Harare.

Jumapili, tarehe 17 Januari, Blantinna Magaya na watoto wake walikuwa wanavua samaki kwa kutumia nyavu kando ya mto wakati ghafla mamba aliruka kutoka kwenye kina kirefu cha mto na kumkamata mguu wake.

Luckmore na Peace hawakuwa na muda wa kufikiria kabla ya kuchukua hatua.

Blantinna Magaya na watoto wake baada ya tukio hilo. Picha: Nyingine

‘’Nilimshika mama yangu na kumkumbatia wakati dada yangu mdogo aliweka mguu juu ya kichwa cha mamba na kupiga macho yake na fimbo,’’ Luckmore alisimulia kwa wakazi wa kijiji baada ya shambulio hilo.

Lakini mnyama huyo hakukubali kushindwa, akitupa mwili wake kwa nguvu mtoni akijaribu kumvuta Magaya zaidi ndani ya mto, lakini watoto walipigana kumuweka mama yao juu ya maji.

‘’Mnyama huyo alikuwa na nguvu sana kiasi cha kutaka kutuvuta sote ndani ya mto,’’ alisema Luckmore.

Kwa bahati nzuri, mamba alianza kuchoka, na kushikilia kwake kwa mama yao mamba akaanza kulegea. Kisha akaachia.

Watoto walikuwa wamechoka lakini walimvuta haraka mama yao kutoka mtoni na kupiga kelele za kuomba msaada.

Katika taarifa kwenye X, Rais Mnangagwa alisema alivutiwa na ujasiri wao.

‘’Nimechukua jukumu la kugharamia ada zao za kielimu na kuwazawadia $5,000 kila mmoja. Hebu tuendeleze ujasiri na huruma kama hii miongoni mwa vijana wetu,’’ aliongeza.

Watoto walipewa zawadi za masomo na pesa taslimu. Picha: Emmerson Mnangagwa

Blantinna Magaya, ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, pia alisifu ujasiri wa watoto wake, akisema, ‘’Sikumbuki chochote kilichotokea wakati watoto hawa waliponiamsha, kile ninachokumbuka ni kuwaona juu yangu wakati nilipokuwa karibu kuvutwa mtoni kwa mara ya tatu na mamba.’’

Hata hivyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori na Hifadhi za Zimbabwe, ZimParks, ilionya kwamba watu wasikaribie miili ya maji inayojulikana kuwa na mamba.

Kulingana na ZimParks, takriban watu 50 waliuawa mwaka 2023, huku wengine 85 wakijeruhiwa katika mashambulizi kama hayo.

TRT Afrika