Machafuko nchini Sudan / Photo: AP

Na Yusuf Dayo

Mzozo unaoendelea nchini Sudan umeonyesha Ulimwengu jinsi uhamishaji wa raia unaweza kuwa suala ngumu wakati mwingine, haya ndiyo baadhi ya mambo kuzingatia kama mgeni wakati wa migogoro.

Mtaalamu wa masuala ya usalama George Msamali, anatupatia mwongozo wa kufuata kwa ajili ya usalama wako.

Tangazo la hatari!

Mataifa mengi huenda yakatoa tangazo kwa wananchi wao kuchukua tahadhari au kuhusu uwezekano wa kutokea vurugu. Huenda likatolewa punde tu baada ya rabsha kuzuka. Tangazo kama hili linakuja na maagizo ya wapi kwa kukimbilia au hatua ya kuchukua iwapo utajikuta umekwama katikati ya makundi hasimu. Tangazo kama hili linasaidia wananchi hao kujiandaa na pia serikali kufanya maandalizi muafaka huku wakitazama hali inavyo badilika.

Njia za mawasiliano

Punde baada ya tangazo la hatari, huenda wakashauri wananchi kukimbilia ubalozini. Ubalozi na majengo yake yote kawaida unaaminiwa kuwa himaya ya nchi husika na wataalamu wa usalama wanashauri kuwa ndio sehemu salama zaidi kuwepo wakati huo na sio rahisi kwa makundi yoyote yanayozozana kushambulia. Pia raia wa kigeni wanatakiwa kupiga simu ubalozini kwao na kujitambulisha waliko, kisha wasubiri maagizo zaidi.

Je utoke au usitoke?

Kwa mujibu wa mtaalamu wa usalama, George Msamali, unatakiwa kutoka nje pale tu umehakikisha ni salama kufanya hivyo. Huenda ikawa punde baada ya kupokea tangazo la hatari, kabla ya kuzuka mapigano au katika muda uliotangazwa wa kusitisha makabiliano uliotangazwa na makundi hasimu. Hata hivyo, iwapo utajikuta tayari umekwama katika makabiliano, ushauri ni ujifungie ndani hapo hapo ulipo hadi waokoaji watakapokufikia. Tofauti na wengi wanavyoamini, hutakiwi kabisa kujaribu kukimbilia mpakani bila kuagizwa na wataalamu.

Tofauti na wengi wanavyoamini, hutakiwi kabisa kujaribu kukimbilia mpakani bila kuagizwa na wataalamu.

George Msamali, Mtaalamu wa Usalama

Uokoaji wa serikali

Punde baada ya kuzuka mapigano, serikali nyingi kawaida huwasiliana na makundi hasimu kuomba nafasi waruhusiwe kuwaondoa wananchi wao walioko huko au kuruhusu msaada wa kibinadamu kupita. Hii inatoa fursa kwao kuwafikia raia wao na kuwaondoa kwa ajili ya usalama.

Hatua za kijeshi

Hatua ya mwisho kabisa ni kuingilia kwa majeshi ya mataifa mengine. Hii inafanyika kama shughuli ya uokoaji inayoongozwa na vikosi maalum, wakati mwingine kwa ushirikiano wa vikosi mbali mbali kutoka mataifa kadhaa na huwaondoa raia wowote wa kigeni watakaye mkuta.

Kuna wakati, japo nadra sana ambapo itifaki hizi za kimataifa zinavunjwa, mfano wapiganaji wa Libya waliposhambulia ubalozi wa Marekani mjini Benghazi mwaka wa 2012, au unaposikia msafara wa msaada wa kibinadamu unashambuliwa. Lakini wataalamu wa usalama wanashauri ni muhimu kufuata utaratibu huu ili kuwa na fursa bora Zaidi ya kuokolewa.

TRT Afrika