Na Abdulwasiu Hassan
Kazi ilisimama ghafla kwa Yakubu Kasim Yakubu, msaidizi wa kiufundi katika kampuni ya mawasiliano ya simu ya Nigeria, mapema mwezi huu wakati muunganisho wa intaneti ulipozimika.
Huko Ghana, Aminu Mohammed pia alikumbana na hitilafu kama hiyo katika benki anakofanyia kazi huku kukiwa na tatizo kubwa la kukatika kwa intaneti.
"Hapo awali hatukuweza kuelewa kinachoendelea. Tulidhani ilikuwa ni hitilafu za kawaida za kuzima kwa mfumo. Kadiri muda ulivyoenda tulifikiri ni suala zito na tulihitaji kulizingatia,” Aminu aliiambia TRT Afrika.
Saa chache baadaye, mdhibiti wa mawasiliano wa Ghana ilitangazia nchi kuwa tatizo lilikuwa kubwa kwenye mfumo. Ilisema waya za chini ya bahari zinazounganisha Afrika Magharibi na Ulaya zimeharibika na kukatika.
Usumbufu wa mtandao pia uliripotiwa katika nchi jirani za eneo la Benin, Burkina Faso, Côte d'Ivoire na hadi Namibia na Afrika Kusini kusini mwa Afrika.
"Chama cha Wanabenki cha Ghana kilijibu kwa niaba ya benki zote nchini, na kuhakikishia ya kwamba miundombinu ya benki bado ni thabiti. Bado unaweza kupata pesa zako,” Aminu alisema.
Waya za chini ya bahari
Waya za chini ya bahari zilizoathiriwa ni West African Cables System (WACS), na Africa Coast to Europe (ACE), MainOne na SAT3.
Waya nyingi za chini ya bahari zinamilikiwa na makampuni ya kibinafsi, huku serikali zikiwa na hisa ndogo.
Barani Afrika, watoa huduma wa huduma za mitandao wa intaneti wanategemea sana waya za chini ya bahari kutoa muunganisho wa intaneti kwa watumiaji, kulingana na Abdullahi Salihu Abubakar, mtaalam wa IT.
Nchini Nigeria, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, kukatika kwa intaneti ziliathiri taasisi kadhaa na makampuni ya biashara.
Hasara ya jumla ya kiuchumi iliyosababishwa na tatizo nchini Nigeria na katika eneo lote bado haijajulikana.
Sababu ya shida ilikuwa kuharibika kwa waya mahali fulani karibu na pwani ya Senegal na Côte d'Ivoire, kulingana na Tume ya Mawasiliano ya Nigeria.
Hakuna sababu ziliyotolewa. MainOne ilisema uharibifu wa waya yake ulitokea pwani ya Afrika Magharibi, na kuongeza kuwa "ilisababishwa na matokeo ya nje."
Kurudisha huduma
Wiki iliyopita, mamlaka ya mawasiliano ya Ghana ilisema itachukua zaidi ya wiki tano kutatua tatizo hilo. Ilisema kipaumbele kitapewa taasisi muhimu kama benki, mitambo ya umeme na maji katika ugawaji wa mtandao wa intaneti.
MainOne ilisema "imebadilisha trafiki" na kwamba kulikuwa na utulivu katika mtandao wake.
Tume ya Mawasiliano ya Nigeria ilisema huduma za sauti na data zilirejeshwa haraka kwa asilimia 90% ya uwezo wa kawaida, ikiongeza kuwa wanaoshughulikia simu wamehakikisha kuwa hali ya kawaida inasubiri kukarabatiwa kwa waya za chini ya bahari zilizoharibika.
Ingawa huduma zilikuwa zimerejeshwa, watumiaji wengi nchini bado wanaripoti huduma duni ya mtandao.
Kuzuia uharibifu
Swali kubwa ni nini kifanyike kuzuia kuvurugika kwa uchumi wa Afrika unaosababishwa na waya zilizoharibika, kwa kuzingatia uwezekano wa uharibifu wa baadaye wa waya hizo, na haliwezi kuzuilika.
Mamlaka ya Kitaifa ya Mawasiliano ya Ghana "ilipendekeza kuwa watoa huduma za kifedha na huduma wanapaswa katika muda wa kati na muda mrefu, kuzingatia kushikilia huduma muhimu ndani ya nchi ili kuhakikisha utoaji wa huduma endelevu endapo kutatokea usumbufu mkubwa."
Wachambuzi wengine wana maoni kwamba taasisi na watu binafsi wanaotegemea intaneti wanapaswa kutoa njia mbadala za mtandao ili kuepuka kukwama endapo kutatokea uharibifu siku zijazo.