Tinubu alishinda uchaguzi wa Februari akiwashinda wapinzani wakuu Atiku Abubakar na Peter Obi. Picha: Getty

Na Abdulwasiu Hassan

Rais mpya wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, anatazamiwa kuapishwa siku ya Jumatatu kumrithi Muhammadu Buhari ambaye anaondoka madarakani baada ya kumaliza mihula yake miwili.

Bw Tinubu, 71, alishinda uchaguzi wa rais wa Nigeria mwezi Februari kwenye jukwaa la chama tawala cha APC. Anakuwa kiongozi wa kumi na sita wa nchi hiyo na rais wa tano aliyechaguliwa kidemokrasia tangu nchi hiyo irejee kwa demokrasia mwaka 1999.

Mwanasiasa huyo mzoefu alifanya kampeni katika rekodi yake ya kuwa gavana wa zamani wa jimbo la Lagos ambako anasifiwa kwa kukuza uchumi wake ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la mapato na maendeleo ya viwanda pamoja na kuboresha mfumo wa usafiri.

Pia alitekeleza miradi ya miundombinu katika kitovu cha kibiashara cha Nigeria ikijumuisha barabara, shule na vituo vya afya.

Hili ndilo linalowapa baadhi ya Wanigeria kama Nasiru Ringim imani na rais mpya. ‘’Tunatumai kuwa kwa fursa hii aliyonayo, ataitumia kuboresha yale aliyofanya siku za nyuma,’’ Ringim aliiambia TRT Afrika. ‘’Naitakia serikali hii mpya mema na tunatumai itatoa,’’ anasema.

Kukuza uchumi

Lakini kazi mpya mbele ya Bola Tinubu na anapokula kiapo cha kuongoza uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na nchi yenye watu wengi zaidi, ni kubwa na matarajio pia ni makubwa.

Tinubu na naibu wake Kashim Shettima wakiwasilisha vyeti vyao vya ushindi wa uchaguzi kwa rais anayeondoka Buhari mwezi Machi. Picha: Reuters

Kiongozi huyo mpya wa Nigeria aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa tayari kutekeleza jukumu hilo. ‘’Nimeburudishwa na niko tayari kwa kazi iliyo mbele yangu,” Tinubu alisema, mara tu baada ya kurejea kutoka safari ya kigeni takriban mwezi mmoja kabla ya kuapishwa kwake.

Kazi inayomngoja Bw Tinubu ‘’inahitaji kufikiri na kuchukua hatua nyingi,’’ anasema Zuhumnan Dapel, mtafiti mwenzake wa masuala ya kiuchumi wa Nigeria katika Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa chenye makao yake Kanada.

‘’Kazi bora zaidi kwa rais mpya ni kuwapa Wanigeria uchumi bora,’’ Bw Zuhumnan aliiambia TRT Afrika.

Alisema Nigeria inatakiwa kuinua uchumi wake kwa kuwekeza zaidi katika sekta zisizo za mafuta ikiwemo kilimo jambo ambalo litasaidia kupunguza uagizaji wa chakula kutoka nje na kukuza mapato ya serikali.

Amir Muhammad Harbo, mkazi wa jimbo la kaskazini la Jigawa anasema anatarajia serikali ya Bola Tinubu kujenga juu ya urithi wa utawala wa Rais Muhammadu Buhari.

‘’Serikali mpya inahitaji kuchukua hatua za kuleta utulivu wa uchumi na kuunda nafasi za kazi,’’ Harbo aliiambia TRT Afrika.

Anaamini kuwa na miradi mingi zaidi kama vile kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta cha Dangote kilichoanzishwa hivi karibuni, kukabiliana na ukosefu wa ajira na kukuza uchumi, maendeleo makubwa nchini Nigeria ‘’yanawezekana.’’

Pia anatoa wito wa kuwepo kwa msingi imara katika sekta ya elimu. ‘’Mfumo wa elimu wa Nigeria unahitaji mageuzi, hasa katika elimu ya msingi,’’ anasema.

Watu katika Soko la Mile 12 mjini Lagos wakifanya biashara kabla ya uzinduzi wa Tinubu. Picha: Reuters

‘’Serikali mpya inahitaji kuwekeza na kuboresha ubora wa elimu kwa Wanigeria wote,’’ Harbo anaongeza. Hii itaifanya nchi kuwa ‘’mahali pazuri zaidi kwa Wanigeria wote.’’

Dk Isa Abdullahi, mkuu wa idara ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Shirikisho Kashere katika jimbo la Gombe anakubali.

Dk Abdullahi anasema serikali mpya ya Nigeria inapaswa kuendelea na juhudi za kufufua na kuunga mkono viwanda vya nchi hiyo ili kuwezesha kupunguza shinikizo kwa serikali kulingana na fursa za ajira.

Hii, anasema, itasaidia uchumi wa nchi unaotegemea mafuta. "Njia pekee ya serikali au jamii inaweza kuzalisha ajira ni kwa uzalishaji," Abdullahi aliiambia TRT Afrika.

"Kama hakuna uzalishaji, hakuna uchumi. Ikiwa hakuna uzalishaji, hakuna ajira. Ikiwa hakuna uzalishaji, hakuna mapato kwa serikali,” anaongeza.

Njia ya utendaji bora

Suala jingine ambalo Nigeria inakabiliana nalo ni ukosefu wa usalama. Katika mahojiano ya hivi majuzi Bola Tinubu alimsifu mtangulizi wake Muhammadu Buhari kwa kulikomesha kundi la Boko Haram ambalo limekuwa likiendesha uasi mbaya kwa zaidi ya muongo mmoja kaskazini mwa nchi hiyo na katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad.

Vikosi vya usalama vya Nigeria vinasema vimeshusha hadhi ya Boko Haram. Picha: AFP.

Pia kuna tatizo la utekaji nyara wa mara kwa mara ili kulipwa fidia na magenge yenye silaha ambayo mamlaka ya Nigeria yamekuwa yakijaribu kukabiliana nayo.

"Kuna haja ya kufanya harambee kati ya mashirika saba ya usalama nchini kwa ajili ya kuimarisha usalama," mchambuzi wa masuala ya usalama Kabiru Adamu aliiambia TRT Afrika.

Wataalamu pia wanaeleza haja ya kustawisha umoja kati ya jumuiya mbalimbali za kikabila na kidini za Nigeria pamoja na kuboresha sekta nyinginezo zikiwemo afya na umeme.

Nigeria mara nyingi inajulikana kama 'jitu la Afrika' kutokana na idadi ya watu, ukubwa wa uchumi na nafasi ya uongozi inayocheza katika masuala ya bara.

Hii kulingana na wachambuzi, ni kiashirio kingine cha changamoto iliyopo mbele ya Bola Tinubu kwani angetarajiwa kutekeleza jukumu hilo muhimu barani Afrika na kwingineko pamoja na kushughulikia maswala ya nyumbani.

Mtafiti, Zuhumnan Dapel, anasema rais mpya wa Nigeria anahitaji ‘’kushirikisha wataalamu’’ kufanya kazi ‘’ kwa uaminifu’’ katika kila sekta. ‘’Akifanya hivi, atafanya vyema,’’ Dapel anahitimisha.

TRT Afrika