Mwanaume apoteza zaidi ya wanafamilia 20 katika shambulio la kijeshi la bahati mbaya Nigeria

Mwanaume apoteza zaidi ya wanafamilia 20 katika shambulio la kijeshi la bahati mbaya Nigeria

Mwanaume mmoja mwenye umri wa makamo amepoteza jamaa 20 hivi katika shambulizi la Jumapili kwenye kijiji kimoja na jeshi la Nigeria
Watoto watatu wa Abdullahi Musa walikuwa miongoni mwa waliouawa katika shambulio la Desemba 3, 2023 katika Jimbo la Kaduna. / Picha: TRT Afrika

Mwanaume mmoja kutoka Nigeria mwenye umri wa makamo amepoteza zaidi ya wanafamilia 20 baada ya jeshi kushambulia raia katika kijiji cha Tudun Biri, katika jimbo la kaskazini la Kaduna siku ya Jumapili.

Abdullahi Musa aliiambia TRT Afrika kwamba siku hiyo alikuwa kwenye sherehe ya kidini asubuhi, wakati mabomu ya kijeshi yalipopiga eneo hilo.

"Nilisikia mlipuko mkubwa, na dakika inayofuata, nilirushwa mbali," alisema akiwa kitandani mwake hospitalini katika Hospitali ya Mafunzo ya Barau Dikko katika Jimbo la Kaduna.

"Kila kitu kilitokea haraka," alikumbuka, akisema alipoteza ufahamu kwa dakika kadhaa.

Watoto Wauawa

Timu za uokoaji wa dharura zilipeleka watu kadhaa waliojeruhiwa hospitalini, wakiwemo Musa.

"Nimejulishwa kuwa watoto wangu watatu waliuawa na shambulio hilo la anga," Musa aliyevunjika moyo alisema.

"Mtoto mmoja alikuwa na furaha sana kuhusu shule, na mara kwa mara aliniambia jinsi mustakabali wake ungekuwa mwangaza. Inavunja moyo wangu kwamba yeye hayupo tena, na hivyo ndivyo kwa watoto wangu wengine," alisema, akiongeza: "Ni mapenzi ya Mungu, nayaheshimu."

Mnusurika huyo alisema kwamba ndugu zake watatu wadogo – ikiwa ni pamoja na mdhamini wa elimu ya watoto wake – walikuwa miongoni mwa waliouawa. Zaidi ya wanafamilia 20 wa jamaa yake walipoteza maisha yao wakati wa shambulio hilo, alisema.

'Inasikitisha na kuumiza'

Watu wasiopungua 85 waliuawa na 66 kujeruhiwa katika shambulio hilo la Jumapili, kulingana na Wakala wa Kitaifa wa Usimamizi wa Dharura wa Nigeria (NEMA).

Rais Bola Tinubu, akielezea tukio hilo kama "baya sana, linalosikitisha, na kuumiza" siku ya Jumanne aliagiza "uchunguzi wa kina na kamili kuhusu tukio hilo."

Siku ya Jumatatu, kamishna wa wizara ya mambo ya ndani ya Jimbo la Kaduna Samuel Aruwan alisema uchunguzi ulibainisha kuwa raia hao waliuawa katika shambulio "lisilokusudiwa na la bahati mbaya."

Kulingana na kamanda wa jeshi, VU Okoro, wanajeshi walikuwa kwenye "doria ya kawaida dhidi ya magaidi" lakini kwa bahati mbaya wakaua raia.

'Walijificha miongoni mwa raia'

Jeshi, kupitia mkurugenzi wa operesheni za vyombo vya habari Meja Jenerali Edward Buba, lilisema kwamba washukiwa wa ugaidi "walijificha miongoni mwa raia", hali iliyosababisha shambulio hilo "linalosikitisha."

Mkuu wa Jeshi la Nigeria Luteni Jenerali Taoreed Lagbaja, aliyetembelea eneo hilo siku ya Jumanne, alisema wanajeshi "walichambua na kutafsiri vibaya mwenendo wa waathiriwa kuwa sawa na ule wa magaidi."

TRT Afrika