Shirika la Ndege la Tanzania, ATCL, limepokea ndege mpya ya BOEING 737-MAX 9 iliyotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam ikitokea Seattle Marekani.
Ndege hiyo mpya ina uwezo wa kuwabeba abiria 181, imewasili chini ya rubani Kiongozi Murtaza Gulamhussein na Rubani Msaidizi Sweetbert Mtweve.
Makamu wa Rais, Tanzania, Philip Mpango alikaribisha ndege hiyo akiwa pamoja na wahusika wengine akiwemo Waziri wa uchukuzi Prof. Makame Mbarawa kwenye sherehe ya kufana iliyoandaliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
"Air Tanzania imechangia pakubwa uboreshaji wa sekta yetu ya utalii. Kati ya 2022-2023, tumeweza kuwapokea watalii 1, 070, 734 ikiwa ni kutoka 106, 138 wa kati ya 2016-2017." Mpango alisema.
"Serikali inaendelea kuboresha huduma za usafiri wa anga ili kuhakikisha zinakidhi ubora unaotakikana wa kimataifa," Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa.
Matindi amesema kuwa ndege hiyo mpya inauwezo wa kuwabeba abiria 181wakiwemo abiria 16 wa daraja la biashara na waliosalia kuwa katika daraja la kawaida.
"Ndege hii ni ya 14 tunayoipokea, zikiwemo 2 kubwa na zingine za masafa ya kati. Na hii ndege itakuwa ni ya tano ya masafa ya kati. Tunatazamia kupokea ndege mbili zaidi na zitawasili mwanzoni mwa mwaka ujao" Matindi alisema.
Mnamo mwezi Juni mwaka huu, Tanzania ilipokea ndege mpya ya mizigo ya Boeing B767-300F yenye uwezo wa kubeba zaidi ya tani 50 na kupokewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.